Oct 16, 2016 07:55 UTC
  • Watu 11 wauawa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati

Watu 11 wameuawa katika shambulio la watu wenye silaha kwenye kambi ya wakimbizi huko Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Kikosi cha kudumisha amani cha Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA) kimeeleza kuwa watu wenye silaha wasiofahamika wameishambulia kambi ya wakimbizi katika eneo la Ngakobo katikati mwa nchi na kuuwa  watu 11 na kujeruhi wengine kumi.

Kikosi cha kudumisha amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA)

Watu waliojeruhiwa tayari wamefikishwa hospitali huko Bambari umbali wa kilomita 300 kutoka mji mkuu  Bangui. Askari wa kofia bluu wa Umoja wa Mataifa na polisi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati hivi sasa wameimarisha usalama katika maeneo ya karibu na kambi hiyo ya wakimbizi baada ya kutokea uvamizi huo na ufyatuaji risasi. Wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ambao nchi yao iliathiriwa na machafuko tangu mwaka 2013, hivi sasa wameanza tena kwa mashaka kurejea katika maisha ya kawaida  baada ya kuingia madarakani serikali mpya; hata hivyo mivutano na machafuko yanayosababishwa na makundi ya wanamgambo wenye silaha vimekuwa kikwazo cha kurejeshwa amani na uthabiti wa kudumu nchini humo.

Tags