Upinzani DRC: Tutaitisha mgomo wa kitaifa na maandamano mengine
Vyama vya upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vimewataka wafanyakazi wote kushirikia mgomo wa kitaifa na maandamano ya nchi nzima siku ya Jumatano, kumshinikiza Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo aachie ngazi mwishoni mwa muhula wake wa pili unaomalizika mwishoni mwa mwaka huu.
Wito wa kufanyika mgomo na maandamano nchini humo ni radiamali ya wapinzani, baada ya chama tawala pamoja na vyama vingine vidogo kukubali kuakhirishwa uchaguzi mkuu hadi Aprili mwaka 2018.
Hapo jana vyama hivyo vilikubaliana kuwa uchaguzi huo uakhirishwe, ili kutoa fursa ya kuandikishwa wapiga kura milioni 10 ambao hawajasajiliwa, kauli ambayo wapinzani wanasema ni ya kuwahadaa wananchi na jamii ya kimataifa.
Hii ni katika hali ambayo, ujumbe wa Jumuiya ya Ustawi ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC umeelekea Kongo DR ili kutathmini hali ya kisiasa na kiusalama, zikiwemo juhudi zinazofanyika kwa shabaha ya kudumisha amani na utulivu wa kisiasa nchini humo. SADC imewataka wapinzani kujiunga na mazungumzo ya kitaifa, ili kufikia mapatano.
Mazungumzo ya kitaifa ya Kongo yalisitishwa baada ya kutokea machafuko ya umwagaji damu tarehe 19 na 20 mwezi Septemba mwaka huu kufuatia maandamano ya wapinzani katika mji mkuu Kinshasa.
Watu 32 waliripotiwa kuuawa katika maandamano hayo ya kuipinga serikali ya Kabila, huku wapinzani wakitaja idadi ya waliouawa kuwa ni watu 100.