Aliyekuwa Makamu wa Rais DRC apatikana na hatia ya kuhonga mashahidi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i17767-aliyekuwa_makamu_wa_rais_drc_apatikana_na_hatia_ya_kuhonga_mashahidi
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imempata na hatia Jean-Pierre Bemba, Makamu wa Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo aliyekuwa akikabiliwa na tuhuma za kutoa rushwa ili kutatiza mkondo wa ushahidi katika kesi dhidi yake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 20, 2016 00:34 UTC
  • Aliyekuwa Makamu wa Rais DRC apatikana na hatia ya kuhonga mashahidi

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imempata na hatia Jean-Pierre Bemba, Makamu wa Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo aliyekuwa akikabiliwa na tuhuma za kutoa rushwa ili kutatiza mkondo wa ushahidi katika kesi dhidi yake.

Aidha mahakama hiyo imewapata na hatia wapambe wanne wa karibu wa Bemba, wakiwemo mawakili wake wawili na mbunge wa zamani wa chama chake, kwa kushirikiana naye kuhujumu mchakato wa sheria.

Akisoma hukumu hiyo jana Jumatano mjini Hague nchini Uholanzi, Jaji wa ICC Bertram Schmitt alisema hakuna mfumo wowote wa sheria duniani unaoweza kukubali kuhongwa mashahidi au kupewa mafunzo ya jinsi ya kutoa ushahidi wa urongo kwa shabaha ya kupotosha au kuangusha kesi.

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC

Jaji Schmitt amesema hukumu hiyo dhidi ya Bemba na wafuasi wake wa karibu inatuma ujumbe wa wazi kuwa, mahakama hiyo katu haitoruhusu kuhujumiwa mkondo wa kesi kwa kuwahonga, kuwapa mafunzo, kuwatishia, kuwahujumu au kuwaua mashahidi.

Mwezi Juni mwaka huu, ICC ilimhukumu Bemba kifungo cha miaka 18 jela, kwa kupatikana na hatia ya kutenda jinai za kivita na dhidi ya binadamu kwa kuwatuma wapiganaji wa MLC katika Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka 2003 ili kusaidia kuzima mapinduzi ya kijeshi dhidi ya rais wa wakati huo, Ange -Felix Patasse.

Mashtaka dhidi ya Jean-Pierre Bemba ambaye hukumu yake ni ya kwanza dhidi ya Makamu wa Rais wa zamani katika mahakama hiyo ya kimataifa iliyobuniwa mwaka 2002, yalijumuisha mauaji na ubakaji.