Viongozi wa Kikristo DRC hawataki kuakhirishwa uchaguzi
Maaskofu wa Kanisa Katoliki katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wametofautiana na uamuzi wa hivi karibuni uliofikiwa na chama tawala pamoja na vyama kadhaa vya upinzani, wa kuakhihirisha uchaguzi mkuu kutoka mwezi ujao hadi Aprili mwaka 2018.
Taarifa ya Baraza la Taifa la Maaskofu wa Katoliki nchini humo imewataka viongozi wote wa kisiasa kuangalia upya makubaliano hayo ya kisiasa yaliyosainiwa Jumanne iliyopita, ili kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika mapema mwaka ujao na Rais Joseph Kabila haruhusiwi kuwania tena kiti hicho kwa muhula wa tatu.
Kadhalika viongozi hao wa Kanisa Katoliki ambalo asilimia 40 ya wananchi wa Kongo DR ni wafuasi wake wametoa wito wa kutoifanyia marekebisho katiba ya nchi wakati huu ambapo nchi hiyo iko kati hali tata.
Hii ni katika hali ambayo, Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema makubaliano hayo ya kisiasa huenda yakatoa mwanga na kuleta anga nzuri ya kuheshimiwa haki za binadamu, mambo ambayo anaamini yatapelekea kufanyika uchaguzi huru, wa haki na wa kidemokrasia mnamo Aprili mwaka 2018.
Chama kikuu cha upinzani nchini humo cha Umoja kwa Ajili ya Demokrasia na Maendeleo ya Kijamii kimesema hakiyatambui makubaliano hayo yaliyotiwa saini baina ya washiriki wa mazungumzo ya kisiasa huko Kinshasa, mji mkuu wa nchi hiyo.
Hali ya taharuki ingali imetanda katika miji kadhaa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hususan mji mkuu Kinshasa, huku wafanyakazi wa sekta mbalimbali wakisusia kazi kufuatia wito wa wapinzani wanaopinga makubaliano hayo ya kisiasa.