Somalia yalalamikia hatua ya Kenya ya kuwati mbaroni wabunge wake
Serikali ya Somalia imelalamikia hatua ya Kenya ya kuwatia mbaroni wabunge wake wanaoishi nchini humo.
Abdisalam Aato, Msemaji wa serikali ya Somalia sanjari na kulalamikia hatua hiyo, ameitaka serikali ya Nairobi kutoa maelezo ya kina kuhusiana na kadhia hiyo. Aato amesema kuwa, hivi karibuni maafisa usalama wa Kenya waliwatia mbaroni wabunge wa Somalia kwa masaa kadhaa, kufuatia hatua ya mbunge mmoja kutowasilisha viza yake kwa maafisa hao. Mazungumzo baina ya Kenya na Somalia yalifanyika siku ya Jumamosi ambapo wabunge kadhaa wa Somalia walioambatana na Omar Abdirashid Ali Sharmarke, Waziri Mkuu wa Somalia aliyeongozana na Baraza lake la Mawaziri, waliwasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi. Katika miaka ya hivi karibuni Kenya na Somalia zimekuwa na mivutano ya kisiasa, licha ya serikali ya Nairobi kwa kushirikiana na baadhi ya nchi za Kiafrika, kutuma askari wake kwa minajili ya kupambana na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la ash-Shabab. Serikali za nchi mbili hizo zimekuwa na mgogoro juu ya mipaka katika maji ya Bahari ya Hindi, huku Kenya ikikabidhi kwa mashirika ya kigeni haki ya kuchimba mafuta na gesi katika eneo linalogombaniwa. Mbali na hayo serikali ya Mogadishu imekuwa ikilalamikia mpango wa serikali ya Nairobi wa kujenga ukuta wa kilometa 700 katika vijiji vya mpaka wa pamoja wa nchi mbili kwa lengo la kuzuia kupenya wanachama wa ash-Shabab nchini Kenya.