Waziri Mkuu wa Somalia atoa hakikisho la kusitishwa mapigano Galkayo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i19786-waziri_mkuu_wa_somalia_atoa_hakikisho_la_kusitishwa_mapigano_galkayo
Waziri Mkuu wa Somalia Omar Sharmarke amesema, amepata hakikisho la kutekelezwa na kuheshimiwa usitishaji vita baina pande hasimu za maeneo ya Galmudug na Puntland.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 19, 2016 12:13 UTC
  • Waziri Mkuu wa Somalia atoa hakikisho la kusitishwa mapigano Galkayo

Waziri Mkuu wa Somalia Omar Sharmarke amesema, amepata hakikisho la kutekelezwa na kuheshimiwa usitishaji vita baina pande hasimu za maeneo ya Galmudug na Puntland.

Sharmarke ametoa tamko hilo leo baada ya kupita wiki mbili tangu makubaliano ya amani yaliyosainiwa na pande hizo mbili kuvunjika na kuzusha mapigano yaliyosababisha watu wasiopungua 29 kuuawa.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Waziri Mkuu wa Somalia imeeleza kuwa Sharmarke alifanya safari wiki iliyopita katika eneo la Galkayo na kufanya mazungumzo ili kuhakikisha usitishaji mapigano unatekelezwa mara moja na kufanya jitihada za kufanikisha mazungumzo ya awali baina ya pande hasimu kwa ajili ya kufikia makubaliano ya amani ya kudumu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Waziri Mkuu wa Somalia alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Abdikarim Hussein Guled wa Galmudug na mwenzake wa Puntland Abdiweli Mohamed Ali na kushuhudia vikosi vya maeneo hayo mawili vikirudi nyuma kutoka eneo la mapigano baina yao hadi eneo la amani la umbali wa kilomita nne.

Rais wa Puntland Abdiweli Mohamed Ali Gaas (kushoto) na mwenzake wa GalMudug Abdikarim Hussein Guled

Akizungumzia mapigano yaliyozuka baada ya kuvunjika makubaliano ya amani, Sharmarke amesema: "Kilichotokea katika kipindi cha mwezi na wiki kadhaa zilizopita huko Galkayo ni kitu cha kusikitisha sana. Ni wajibu wetu sote tuliopo hapa na wasiokuwepo hapa kuhakikisha hakitokei tena".

Galmudug na Puntland ambayo ni maeneo ya Somalia yanayojiendeshea masuala yao ya ndani zina historia ya kupigana ambapo duru ya karibuni ya mapigano imetokea wiki mbili zilizopita baada ya kuzuka mzozo juu ya umiliki wa majengo katika mji wa Galkayo ambao umegawika sehemu mbili, moja ikiwa katika eneo la Galmudug na nyingine katika upande wa Puntland.../