Al Shabab 11 wauliwa kusini mwa Somalia
Wanamgambo 11 wa kundi la al Shabab lenye makao yake nchini Somalia wameuawa na vikosi vya jeshi la serikali kusini mwa nchi hiyo.
Mohamed Isak Hassan Kamishna Maalumu wa polisi wa eneo la kusini magharibi mwa Somalia amewaambia waandishi wa habari kuwa jeshi la nchi hiyo jana lilifanikiwa kuwauwa wanachama 11 wa al Shabab kufutia mapigano yaliyojiri kati ya jeshi hilo na kundi la al Shabab katika kijiji cha Gof-Gadud kusini mwa Somalia. Mohamed Isak Hassan amesema kuwa jeshi la Somalia limepoteza wanajeshi wake watatu katika mapigano hayo na wengine wawili wamejeruhiwa vibaya.
Kamishna Maalumu wa polisi wa eneo la kusini magharibi mwa Somalia amesisitiza kuwa jeshi la Somalia limedhamiria kwa dhati kushadidisha mashambulizi dhidi ya al Shabab na kuliangamiza kundi hilo kwa kushirikiana na kikosi cha kudumisha amani cha Umoja wa Afrika. Yapata karibu miaka 25 sasa ambapo Somalia inakabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya wanamgambo wa kundi la al Shabab. Wanajeshi wa nchi za Kiafrika karibu elfu 22 wametumwa Somalia kupambana na al Shabab tangu mwaka 2007.