Mahakama ya Nigeria yatoa amri ya kuachiwa huru Sheikh Zakzaky
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i20680-mahakama_ya_nigeria_yatoa_amri_ya_kuachiwa_huru_sheikh_zakzaky
Hatimaye na baada ya kupita zaidi ya mwaka mmoja tangu kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky atiwe nguvuni, mahakama ya nchi hiyo imetoa amri ya kuachiwa huru mara mmoja kiongozi huyo.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Dec 03, 2016 12:50 UTC
  • Sheikh Ibrahim Zakzaky
    Sheikh Ibrahim Zakzaky

Hatimaye na baada ya kupita zaidi ya mwaka mmoja tangu kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky atiwe nguvuni, mahakama ya nchi hiyo imetoa amri ya kuachiwa huru mara mmoja kiongozi huyo.

Jaji Gabriel Kolawole wa kitengo cha Abuja cha Mahakama Kuu ya Nigeria ameiamuru serikali kumwachilia huru bila ya masharti yoyote Sheikh Zakzaky na mke wake katika kipindi cha siku 45 zijazo.

Hukumu ya mahakama hiyo imesema kuwa, kuendelea kushikiliwa Sheikh Zakzaky gerezani bila ya kufikishwa mahakamani ni kukiuka haki zake zinazosisitizwa katika katiba ya Nigeria na kwamba madai ya serikali kwamba inamshikilia Sheikh Zakzaky gerezani kwa shabaha ya kulinda usalama wake na mkewe, hayawezi kukubalika. 

Baada ya kutolewa hukumu hiyo, wakili wa Sheikh Ibrahim Zakzaky amepongeza uamuzi huo na kueleza kuwa, ana matumaini hukumu hiyo itakuwa ishara kwamba, serikali ya Abuja imekomesha ukatili na ukandamiza dhidi ya Waislamu.

Vijana wengi wa Kiislamu wameuawa katika hujuma za jeshi la Nigeria

Sheikh Ibrahim Zakzaky na mke wake walikamatwa na kufungwa gerezani siku moja baada ya jeshi la Nigeria kushambulia kituo cha kidini cha Husainiya ya Baqiyyatullah katika mji wa Zaria na kuua mamia ya Waislamu. Wakati huo Sheikh Zakzaky alipigwa na kudhalilishwa na kupoteza jicho lake moja. Vilevile kiongozi huyo wa kidini amepooza baadhi ya viungo vya mwili kutokana na mateso na kutelekezwa gerezani bila ya kupewa matibabu. Watoto watatu wa kiongozi huyo pia waliuawa shahidi katika mauaji hayo. Tangu wakati huo serikali ya Nigeria ilizidisha mashinikizo dhidi ya Waislamu hususan wa madhehebu ya Shia ambao wamekuwa wakishambuliwa na kusumbuliwa mara kwa mara na jeshi la Nigeria.

Mauaji ya Waislamu Zaria baada ya jeshi la Nigeria kushambulia Husseiniyya ya Baqiyatullah 

Mashinikizo dhidi ya Waislamu wa Nigeria yameongezeka ilhali katika kipindi chote cha miongo kadhaa iliyopita wafuasi wa dini hiyo wamekuwa wakiishi kwa amani na utulivu na raia wengine wa nchi hiyo. Katika miaka ya hivi karibuni kufuatia mabadiliko yaliyotokea katika baadhi ya nchi za Afrika na kufeli kwa siasa za baadhi ya nchi kama Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni wa Israel za kutaka kupanua ushawishi wao barani humo, tawala hizo zilizidisha mikakati ya kutaka kuwa na satua zaidi katika nchi za Afrika kwa kutumia njia ya kuyasaidia na kuyaunga mkono magenge yenye misimamo mikali kama kundi la Kiwahabi. Inasikitisha kuona kwamba, maamuzi yaliyochukuliwa na baadhi ya serikali za nchi za Kiafrika kama Nigeria pia yamezidisha mashinikizo dhidi ya Waislamu na kuwapa ruhusa wanajeshi na vyombo vya usalama kuwakandamiza wafuasi wa dini hiyo au kutunga sheria kali dhidi yao. Kwa mfano tu siku chache zilizopita gavana wa jimbo la Kano nchini Nigeria alitoa amri ya kupiga marufuku shughuli za aina yoyote au mikusanyiko ya kidini katika jimbo hilo. Maamuzi kama haya yanatumiwa vibaya na jeshi la Nigeria kufanya ukatili na ukandamizaji dhidi ya Waislamu wanaokuwa katika shughuli za kiibada na kidini.

Waislamu wa Kano, Nigeria wakiwa katika shughuli ya kidini

Licha ya sheria na maamuzi hayo yote, Waislamu wa Nigeria wameendelea kukusanyika na kufanya maandamano katika miji mbalimbali ya nchi hiyo wakitaka kuachiwa huru kiongozi wao, Sheikh Ibrahim Zakzaky na wanaharakati wengine wanaoshikiliwa katika korokoro za nchi hiyo.

Kwa vyovyote vile hukumu na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Nigeria iliyoamuru kuachiwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky tena bila ya masharti yoyote, ni ushahidi kwamba, kiongozi huyo na wenzake walikamatwa bila ya kosa, na kuna ulazima wa kuchukuliwa hatua na kuwawajibisha wale wote waliohusika katika uhalifu huo na kuhakikisha kwamba damu za mamia ya Waislamu waliouawa bila ya hatia, hazipotei bure.