Wananchi wa Ghana wapiga kura kumchagua Rais na Wabunge
Wananchi wa Ghana leo wameelekea kwenye masanduku ya kupigia kura kumchagua Rais Mpya na wawakilishi wa bunge.
Uchaguzi huo umeanza leo kote nchini kote chini ya mamia ya waangalizi wa uchaguzi kutoka nchi za nje. Jumla ya wagombea saba kutoka vyama mbalimbali huko Ghana wamechuana katika uchaguzi wa leo wa rais kuwania kiti cha Rais huku wagombea 1158 wakichuana kwa ajili ya kuwania viti vya uwakilishi bungeni.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ghana imetangaza kuwa wananchi karibu milioni 16 wameshiriki katika uchaguzi huo wa leo wa Rais na Bunge. Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo pia imetangaza kuwa waangalizi wa nchi za nje zaidi ya 400 na elfu 12 wa ndani wamesimamia mchakato wa uchaguzi. Vituo vya kupigia kura karibu 29 vimeandaliwa huko Ghana ili kuhakikisha kuwa uchaguzi huu unafanyika.
Wakati huo huo wanaharakati wa kisiasa nchini Ghana wamesisitiza juu ya kuzuiwa aina yoyote ya ghasia na machafuko kutoka kwa wafuasi wa wagombea wa uchaguzi na kutaka kudhaminiwa kikamilifu ulinzi na usalama, kufanyika uchaguzi huru na wa haki na kuzingatiwa madai ya kisheria ya wanaharakati wote wa kisiasa.
Rais wa hivi sasa wa Ghana John Dramani Mahama ambaye alishika hatamu za kuiongoza nchi iyo mwaka 2013 baada ya kuaga dunia Rais John Atta Mills, amechuana leo kugombea kiti cha urais na Nana Akufo-Addo mgombea kutoka chama cha New Patriotic ambaye alishindwa katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2012.