Rais wa Somalia: Nilinukuliwa vibaya kuhusu idadi ya waliouawa El-Adde
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i2098-rais_wa_somalia_nilinukuliwa_vibaya_kuhusu_idadi_ya_waliouawa_el_adde
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud amesema alinukuliwa vibaya na vyombo vya habari kuhusu idadi ya askari wa Jeshi la Ulinzi la Kenya KDF waliouawa mwezi uliopita katika hujuma ya kundi la al-Shabab katika kambi ya El-Adde.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 28, 2016 04:36 UTC
  • Rais wa Somalia: Nilinukuliwa vibaya kuhusu idadi ya waliouawa El-Adde

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud amesema alinukuliwa vibaya na vyombo vya habari kuhusu idadi ya askari wa Jeshi la Ulinzi la Kenya KDF waliouawa mwezi uliopita katika hujuma ya kundi la al-Shabab katika kambi ya El-Adde.

Daud Aweis, Msemaji wa Rais Mohamud wa Somalia amepuuzilia mbali kile kilichotajwa kuwa kauli ya rais, kwamba askari 200 wa Kenya waliuawa katika hujuma hiyo ya El-Adde. Amesema kuwa rais wa Somalia alikusudia kuwa kambi ya El-Adde ilikuwa na jumla ya askari kati ya 180 na 200 wa Kenya, lakini hakumaanisha kuwa wote waliuawa. Msemaji wa Rais wa Somalia ameongeza kuwa, Somalia inathamini mchango unaotolewa na Kenya katika kuhakikisha kuwa amani na usalama unarejea katika nchi hiyo ya pembe ya Afrika. Hata hivyo taarifa hiyo ya Msemaji wa Rais wa Somalia haijataja idadi ya askari wa KDF waliouawa katika hujuma hiyo. Awali, Msemaji wa jeshi la Kenya, Kanali David Obonyo alipuuzilia mbali idadi hiyo iliyodaiwa kutolewa na Rais wa Somalia akisisitiza kuwa takwimu hizo hazijatolewa na Kenya wala ofisa yoyote wa serikali ya Nairobi. Aidha jeshi la Kenya halijatoa idadi rasmi ya wanajeshi wake waliouawa katika hujuma hiyo ya mwezi uliopita wa Januari. Kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab ambalo siku chache zilizopita lilitoa kanda ya video inayoonyesha athari za mashambulizi ya El-Adde, lilidai kuwa liliua wanajeshi zaidi ya 100 wa Kenya katika hujuma hiyo.