Madaktari na wauguzi Kenya watishia kupanua wigo wa mgomo wao
Madaktari na wauguzi wa hospitali za serikali nchini Kenya ambao wanaingia katika siku yao ya tano ya mgomo wao wametishia kuwa watapanua wigo wa mgomo huo endapo serikali haitasikiliza matakwa yao.
Madaktari na wauguzi hao wamesema kuwa, watapanua wigo wa mgomo wao hadi katika hospitali binafsi endapo serikali ya Rais Uhuru Kenyatta haitachukua hatua za lazima za kushughulikia matakwa yao.
Tishio hilo la madaktari na wauguzi wa hospitali za umma limetolewa baada ya kutokuwa na natija mazungumzo ya madaktari na wauguzi wa hospitali za serikali za mji mkuu Nairobi.
Mgomo huo umeathiri huduma kwenye hospitali za umma huku wafanyakazi wa sekta ya umma wakidai kuwa lazima serikali iheshimu utekelezaji wa mkataba uliotiwa sahihi mwaka 2013. Wagonjwa zaidi ya 20 wameshafiriki dunia tangu mgomo huo ulipoanza Jumatatu iliyopita.
Muungano wa Madaktari na Wauguzi Kenya ambao una wanachama wapatao elfu tano umeeleza kuwa, makubaliano hayo ya malipo yalipasa kuwapatia nyongeza ya mshahara ya asilimia 300, kujadili mazingira yao ya utendaji kazi na mifumo ya kazi, kuangalia upya vigezo vya kupandishwa cheo na kutatua tatizo la uhaba wa wafanyakazi wa huduma za afya mahospitalini.
Wakati huo huo, chama cha madaktari nchini Kenya kimetangaza kuwa hospitali zote zikiwemo za binafsi zitagoma kwa masaa 24 siku ya Jumanne tarahe 13 mwezi huu, ikiwa serikali itashindwa kutekeleza makubaliano ya kuongeza mishahara ya wafanyakazi wa sekta ya afya na kuboresha mazingira yao ya kazi.