Wakimbizi waliofukuzwa Algeria waingia nchini Niger
(last modified Sat, 10 Dec 2016 13:56:27 GMT )
Dec 10, 2016 13:56 UTC
  • Wakimbizi waliofukuzwa Algeria waingia nchini Niger

Mamia ya wakimbizi wa Kiafrika waliofukuzwa nchini Algeria wameingia katika nchi jirani ya Niger.

Vyombo vya habari vimeripoti habari hiyo na kuwanukuu mashuhuda wakisema kuwa, wakimbizi hao kutoka nchi za Niger, Mali, Guinea na Senegal wameingia nchini Niger kwa kutumia malori matano ya Algeria yaliongozwa na vikosi vya usalama vya Niger. Wakimbizi hao wameingia katika mji wa Agadez wa katikati mwa Niger na kuhifadhiwa kwenye uwanja wa mpira wa mji huo.

Wakimbizi wakishuka kwenye malori nchini Niger

 

Waziri Mkuu wa Niger Brigi Rafini amethibitisha habari hiyo na kusema kuwa, opereseheni hiyo imefanyika kwa idhini ya viongozi wa nchi hiyo.

Habari zinasema kuwa wakimbizi hao ni wahanga wa operesheni kubwa ya viongozi wa Algeria ambao wameanzisha kampeni maalumu ya kuwarejesha makwao wakimbizi wote walioko nchini humo. Ikumbukwe kuwa mwaka 2014 pia, wakimbizi elfu tatu wa Niger walirejeshwa nchini kwao kutoka Algeria.

Vile vile mwezi Oktoba 2013, raia 92 wa Niger wakiwemo watoto wadogo 52 na wanawake 33 wakazi wa eneo la Zinder la kusini mwa Niger walipoteza maisha katika mpaka wa nchi hiyo na Algeria baada ya maafisa wa Algeria kuwapiga marufuku kuingia kwenye ardhi ya nchi hiyo.

 

Tags