Kikao cha viongozi wa IGAD cha kujadili amani ya eneo
Viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ustawi wa Mashariki mwa Afrika IGAD wamekutana katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa kwa kikao cha 29 cha dharura ambacho kimefanyika kwa uenyekiti wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo Hailemariam Desalegn kujadili amani na uthabiti wa eneo hasa katika nchi za Sudan Kusini na Somalia.
Akihutubia kikao hicho, Waziri Mkuu wa Ethiopia amesema kufuatia operesheni kadhaa za kijeshi zilizofanyika kwa mafanikio pamoja na juhudi za mtawalia zinazofanyika kwa ajili ya kuunda serikali nchini Somalia, amani na uthabiti umeendelea kuboreka hatua kwa hatua nchini humo; lakini uwepo wa kundi la Al-Shabaab ungali ni changamoto muhimu kwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa Desalegn, tatizo kuu katika kukabiliana na Al-Shabaab ni kutokuwepo uratibu baina ya vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika Kusini nchini Somalia, AMISOM, vikosi vingine rafiki pamoja na vikosi vya jeshi la taifa la Somalia.
Kikao cha 29 cha dharura cha viongozi wa nchi wanachama wa IGAD ambacho kilifanyika siku ya Ijumaa, kilihudhuriwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Marais wa Sudan, Sudan Kusini, Djibouti na Somalia pamoja na mawaziri wa Mambo ya Nje wa Kenya na Uganda.
Hivi sasa nchi nyingi za eneo la Mashariki na Pembe ya Afrika zinakabiliwa na changamoto za usalama, za kiuchumi na kisiasa. Japokuwa mapambano ya kulitokomeza kundi la kigaidi na kitakfiri la Al-Shabaab nchini Somalia zimepata mafanikio kadhaa lakini mashambulio yanayoendelea kufanywa na kundi hilo yangali ni kikwazo cha kurejesha amani kamili katika eneo.
Kundi la Al- Shabaab ambalo ni muitifaki wa mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda lilianzisha vita mwaka 2007 kwa lengo la kuiangusha serikali ya Somalia. Hata hivyo baada ya kushikilia kwa muda maeneo kadhaa muhimu ya ardhi ya nchi hiyo hatimaye mwaka 2011 lilipoteza udhibiti katika maeneo ya kati na ngome zake nyingine kadhaa ukiwemo mji wa Afgoowe ulioko kusini magharibi mwa nchi hiyo. Aidha licha ya kupita miaka mitano sasa tangu kundi hilo la kigaidi na kitakfiri litimuliwe katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu lakini lingali linaendeleza mashambulio dhidi ya vikosi vya serikali, raia pamoja na vikosi vya AMISOM.
Mbali na suala la usalama wa Somalia, kikao cha dharura cha wakuu wa nchi wanachama wa IGAD kilijadili pia maandalizi ya uchaguzi wa nchi hiyo ambao ulikuwa ulifanyike wiki kadhaa nyuma lakini ukaahirishwa siku moja tu kabla ya tarehe ya kufanyika kwake. Uchaguzi huo sasa umepangwa kufanyika tarehe 28 ya mwezi huu wa Desemba, lakini kungali kuna matatizo na changamoto kadhaa huku mjadala kuhusu uwezekano wa kufanyika udanganyifu, uchakachuaji wa matokeo pamoja na kutolewa vitisho kwa wapiga kura na kukosekana usalama bado haujamalizika.
Mbali na Somalia, wakuu wa jumuiya ya IGAD walichunguza pia hali mbaya ya mgogoro wa kisiasa unaoendelea kushuhudiwa nchini Sudan Kusini, kiasi kwamba Umoja wa Mataifa umetangaza kupitia taarifa kuwa Baraza la Haki za Binadamu la umoja huo litafanya kikao cha dharura tarehe 14 mwezi huu kujadili hali ya nchi hiyo. Kikao hicho kinaitishwa kwa ombi la nchi zipatazo 40. Ujumbe wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ulieleza baada ya safari yake ya siku 10 nchini Sudan Kusini kwamba kuna uangamizaji wa kikabila unaofanyika katika baadhi ya maeneo na kwamba kuna viashiria vya kutokea mauaji ya kimbari nchini humo kama yale yaliyoshuhudiwa mwaka 1994 nchini Rwanda.
Mbali na matatizo hayo, suala la ukame na hali mbaya ya uhaba wa chakula ni maafa mengine yanayoikabili nchi hiyo. Katika ripoti yake ya mwezi Novemba, Umoja wa Mataifa ulitoa wito kwa jamii ya kimataifa kuwasaidia watu wa eneo la Pembe ya Afrika na kusisitiza kuwa watu wasiopungua milioni 29 katika eneo hilo wanahitajia msaada wa chakula. Inakadiriwa kuwa hali ya uhaba wa chakula katika maeneo ya nchi mbalimbali zenye migogoro ikiwemo Somalia, Sudan Kusini na Burundi, pamoja na maeneo ambayo wastani wa mvua za mtawalia za msimu ulikuwa wa kiwango cha chini itakuwa mbaya zaidi.
Nchi washiriki wa kikao cha 29 cha dharura cha Jumuiya ya Ustawi wa Mashariki mwa Afrika IGAD zimesema zina matumaini kuwa kuimarishwa ushirikiano wa kieneo na kupatikana njia za ufumbuzi wa kisiasa kutawezesha kuitatua migogoro iliyopo hivi sasa katika eneo hilo…/