Dec 14, 2016 14:17 UTC
  • Watoto laki 4 katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na njaa Nigeria

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umetahadharisha kuwa mamia ya maelfu ya watoto nchini Nigeria wako katika hatari ya kuaga dunia kutokana na vita, njaa na lishe duni.

Anthony Lake, Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF amesema eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria linashuhudia mgogoro mkubwa wa kibinadamu na kwamba watoto laki 4 wanakabiliwa na hatari ya kupoteza maisha kutokana na baa la njaa.

Baa la njaa linawakabili mamia ya maelfu ya watoto Nigeria

Amesema huenda watoto 80,000 wakafariki dunia katika miezi michache ijayo kutokana na makali ya njaa katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa.

Ripoti ya Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa imesema kuwa maeneo yanayodhibitiwa na kundi la kigaidi la Boko Haram yana idadi ya watu milioni 14 wanaohitajia msaada wa kibinadamu na kwamba kuna hatari ya watoto 17 elfu kupoteza maisha eneo la kaskazini mashariki mwa nchi mwaka 2017.

Tokea Boko Haram ianzishe uasi wake Nigeria mwaka 2009, watu zaidi ya elfu 20 wamepoteza maisha. Aidha zaidi ya watu milioni mbili wamefanywa wakimbizi kufuatia ugaidi wa Boko Haram hususan katika maeneo ya Borno, Adamawa na Yobe.

Magaidi wa Boko Haram

 

Tags