Mamia ya raia wakombolewa kutoka mikononi mwa Boko Haram, Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i21457-mamia_ya_raia_wakombolewa_kutoka_mikononi_mwa_boko_haram_nigeria
Afisa wa jeshi la Nigeria amesema kuwa, zaidi ya raia 600 wakiwemo watoto 450 wa nchi hiyo wamekombolewa kutoka mikononi mwa kundi la kigaidi la Boko Haram.
(last modified 2026-02-22T02:21:18+00:00 )
Dec 15, 2016 06:21 UTC
  • Mamia ya raia wakombolewa kutoka mikononi mwa Boko Haram, Nigeria

Afisa wa jeshi la Nigeria amesema kuwa, zaidi ya raia 600 wakiwemo watoto 450 wa nchi hiyo wamekombolewa kutoka mikononi mwa kundi la kigaidi la Boko Haram.

Lucky Irabor amesema kuwa, makumi ya wapiganaji wa kundi la Boko Haram wameangamizwa katika operesheni iliyofanywa na jeshi katika msitu wa Sambisa kwa ajili ya kukomboa raia hao. 

Siku chache zilizopita Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Afrika ya Kati, aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa, licha ya kuwa magaidi hao wamekimbia eneo la Ziwa Chad baada ya kufurushwa na kikosi cha askari wa nchi za kanda hiyo, lakini kundi hilo la kigaidi bado ni tishio kwa usalama wa eneo hilo.

Raia waliokombolewa Nigeria

Kundi la kigaidi la Boko Haram limekuwa likiendesha mashambulizi ya kutisha na mauaji ya raia katika nchi za Nigeria, Cameroon, Chad na Niger kwa miaka kadhaa sasa. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa mashambulio ya Boko Haram nchini Nigeria yameua zaidi ya watu elfu ishirini na kuwalazimisha wengine milioni mbili na laki sita kuwa wakimbizi.