Milipuko ya kigaidi yaendelea kuitikisa Somalia, wanajeshi watano wauliwa
Wanajeshi watano wa Somalia wameuawa katika mlipuko wa bomu la kutegwa garini uliotekelezwa leo karibu na ikulu ya Rais wa Somalia na kujeruhi pia makumi ya watu.
Polisi ya Somalia imetangaza kuwa gari moja lililokuwa limetegwa bomu ndani yake liliripuka umbali wa kilomita 500 kutoka ikulu ya Rais huko Mogadishu na kujeruhi makumi ya watu. Afisa mmoja wa polisi ya Somalia amealiambia Shirika la Habari la Reuters kuwa mtu aliyefanya hujuma hiyo, alilipua gari hilo lililokuwa limetegwa bomu ndani yake baada ya polisi kumuamuru asimame katika kituo cha upekuzi.
Hadi sasa haijafahamika ni watu au kundi lipi lililohusika na mlipuko huo karibu na ikulu ya Rais wa Somalia hii leo? Hata hivyo kundi la kigaidi la al Shabab lenye makao yake Somalia katika siku za hivi karibuni limezidisha mashambulizi yake katika maeneo mbalimbali ya mji mkuu Mogadishu.
Itakumbukwa kuwa, watu zaidi ya 100 waliuawa katika mashambulizi matatu yaliyofanywa na al Shabab katika muda wa siku moja katika lango la kuingilia bandari kuu ya Mogadishu hivi majuzi.