Rwanda yataka kupatiwa ufumbuzi mgogoro na jirani yake, Burundi
Rais Paul Kagame wa Rwanda amesema kuwa, nchi yake inataka kupatiwa ufumbuzi mgogoro na jirani yake Burundi kupitia njia ya mazungumzo
Rais Kagame amesema kuwa, nchi yake inatoa kipaumbele kwa suala la kupatiwa ufumbuzi mvutano kati yake na Burundi kupitia njia ya mazungumzo.
Rais Kagame amesema hayo katika mazungumzo yake na waandishi wa habari mjini Kigali na kueleza kuwa, wakati ambapo kuna watu wanaorahisisha mazungumzo na wanachukua hatua kuhakikisha kwamba, hitialfu kati ya Rwanda na Burundi zinaondika, hii ina maana kwamba, mazungumzo ya kuupatia ufumbuzi mgogoro huu yanasonga mbele.
Hitilafu na mivutano ya kisiasa kati ya nchi za Rwanda na Burundi ilipamba moto tena hivi karibuni baada ya kuuawa raia mmoja wa Burundi katika eneo la mpaka wa nchi hizo mbili.
Uhusiano wa nchi hizo mbili jirani umepooza na kuzorota tangu ulipoanza mgogoro wa ndani wa Burundi Aprili mwaka jana.
Maafisa wa serikali ya Burundi wanaituhumu Rwanda kuwa inawasaidia na kuwaunga mkono waasi wanaotaka kuiondoa madarakani serikali ya Rais Nkurunziza.
Tangu ulipozuka mgogoro wa kisiasa kati ya nchi hizo mbili jirani Burundi ilichukua uamuzi kupunguza kiwango cha biashara na Rwanda.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, kwa kutilia maanani muundo wa kijamii unaoshabihiana kati ya nchi mbili jirani za Burundi na Rwanda, kuna wasiwasi kuwa, iwapo mgogoro wa ndani nchini Burundi utapanuka na kushadidi zaidi yumkini ukaiathiri kwa kiwango kikubwa nchi jirani ya Rwanda.