Hali ya kulegalega kisiasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i21862-hali_ya_kulegalega_kisiasa_katika_jamhuri_ya_kidemokrasia_ya_congo
Sambamba na kumalizika muhula wa kisheria wa uongozi wa Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, mji mkuu Kinshasa na miji mingine ya nchi hiyo imeshuhudia taswira ya kuimarisha usalama karibu katika kila kona.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 21, 2016 13:22 UTC
  • Hali ya kulegalega kisiasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Sambamba na kumalizika muhula wa kisheria wa uongozi wa Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, mji mkuu Kinshasa na miji mingine ya nchi hiyo imeshuhudia taswira ya kuimarisha usalama karibu katika kila kona.

Wananchi wanaopinga Rais Kabila kuendelea kubakia madarakani, wamemiminika katika mitaa na barabara za miji mbalimbali ya hiyo hususan Kinshasa na kufanya maandamano wakitaka kiongozi huyo aondoke madarakani.

Maandamano hayo yamegeuka na kuwa uwanja wa mapambano baina ya raia na vyombo vya usalama ambapo baadhi ya ripoti zinasema kuwa, watu wasiopungua 20 wameshauawa katika vurugu na machafuko hayo. Ikiwa ni masaa machache tu baada ya kumalizika muhula wake wa uongozi, Rais Kabila alitangaza habari ya kuundwa serikali mpya. Rais Kabila alichukua hatua hiyo bila kusubiri natija ya mazungumzo ya kisiasa kati ya wawakilishi wa serikali na wapinzani yaliyokuwa yakifanyika mjini Kinshasa.

Joseph Kabila, ambaye muhula wake wa uongozi umemalizika

Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo muhula wa uongozi wa Rais Kabila ulimalizika jana tarehe 20 Desemba na kwa mujibu wa katiba hiyo, Kabila haruhusiwi kugombea kiti cha urais katika uchaguzi ujao kutokana na kuwa ameshaiongoza nchi hiyo kwa mihula miwili.

Wapinzani wa Rais Kabila wanaamini kwamba, baada ya tarehe 20 Desemba yaani Jumanne ya jana, kiongozi huyo hana uhalali wa kuiongoza tena nchi hiyo. Ni kwa miezi kadhaa sasa ambapo mivutano ya kisiasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekuwa ikishuhudiwa. Wapinzani katika nchi hiyo wanataka Rais Kabila akae kando kwa mujibu wa Katiba. Hata hivyo baada ya uchaguzi wa DRC kuakhirishwa Rais Kabila anaonekana kuendelea kubakia madarakani, jambo ambalo linapingwa vikali na wapinzani. Vyama vya upinzani vinaamini kwamba, Rais Kabila hapaswi kuweko hata katika serikali ya mpito itakayoongoza hadi uchaguzi ujao utakapofanyika. 

Hata kama tarehe hasa ya kufanyika uchaguzi ujao nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo bado haijajulikana lakini baada ya mashinikizo ya fikra za waliowengi, Tume ya Uchaguzi ya DRC ilitangaza kuwa, uchaguzi huo utafanyika Disemba 2018.  Kutokuweko bajeti ya kutosha ya kuendeshea zoezi la uchaguzi huo na kukosekana anga mwafaka ya uchaguzi ni miongoni mwa sababu zilizotajwa na Tume ya Uchaguzi ya DRC kwa ajili ya kuakhirisha uchaguzi huo.

Usalama umeimarishwa katika miji yote

Hata hivyo wapinzani wa nchi hiyo wanasema kuwa, sababu hizo ni visingizo tu vya kutaka kumbakisha madarakani Rais Kabila na hivyo kumuandalia mazingira ya kubadilisha Katiba na kuendelea kutawala nchi. Wapinzania wanataka Kabila aachie ngazi na kuundwe serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa ambayo itakuwa na jukumu pia la kuandaa na kuitisha uchaguzi ujao. Mwendo wa kinyonga wa marekebisho pamoja na kupuuzwa harakati za kijamii  za vyama vya upinzani ni mambo mengine yanayolalamikiwa na wapinzani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. 

Kushika kasi mivutano ya kisiasa katika nchi hiyo sambamba na kuongezeka wimbi la vitisho kumekwamisha juhudi zote za ndani na nje za kufikiwa mwafaka baina ya serikali na vyama vya upinzani vya nchi hiyo. Mara hii pia licha ya kuweko juhudi kama hizo na hata kuendelea mazungumzo ya kufikiwa mwafaka baina ya serikali na wapinzani yaliyokuwa yakifanyika kwa upatanishi wa kanisa katoliki, walimwengu wameshuhudia Kabila akitangaza kuundwa serikali mpya na kutosubiri natija ya mazungumzo hayo.

Mandamano ya wapinzani DRC

Baraza hilo jipya la mawaziri linaongozwa na Waziri Mkuu Samy Badibanga. Kambi kuu ya upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inayoongozwa na Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS), Etienne Tshisekedi imewataka wananchi kutomtambua tena Joseph Kabila kama rais wa nchi hiyo na imewahimiza kuonesha upinzani wao dhidi ya Kabila kwa njia ya amani ili aachie madaraka ya nchi.

Hapana shaka kuwa, kuendelea mvutano wa sasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kunatia wasiwasi wa uwezekano wa nchi hiyo kutumbukia katika vita na machafuko ya ndani.