Ethiopia yawaachia huru watu karibu elfu 10 'waliokiuka hali ya hatari'
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i21874-ethiopia_yawaachia_huru_watu_karibu_elfu_10_'waliokiuka_hali_ya_hatari'
Serikali ya Ethiopia imewaachia huru takriban watu elfu 10 waliokamatwa chini ya anga ya hali ya hatari lakini inapania kuwapandisha kizimbani maelfu ya wengine wanaotuhumiwa kuhujumu usalama wa taifa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 21, 2016 14:33 UTC
  • Ethiopia yawaachia huru watu karibu elfu 10 'waliokiuka hali ya hatari'

Serikali ya Ethiopia imewaachia huru takriban watu elfu 10 waliokamatwa chini ya anga ya hali ya hatari lakini inapania kuwapandisha kizimbani maelfu ya wengine wanaotuhumiwa kuhujumu usalama wa taifa.

Zadig Abraha, naibu msemaji wa serikali ya Ethiopia amesema kuwa, watu 9,800 wameachiwa huru leo Jumatano na kwamba serikali inapanga kuwafunguliwa mashtaka wengine 2,500 wanaodaiwa kuchochea ghasia nchini humo.

Amesema walioachiwa huru wamepokea mafunzo mbali mbali walipokuwa kizuizini na serikali inatumai kuwa, hawatajihusisha tena na uvunjaji wa sheria na kushiriki maandamano ambayo hayana kibali.

Maandamano dhidi ya serikali nchini Ethiopia

Duru za habari zinaarifu kuwa, aghalabu ya waliokamatwa katika kipindi cha hali ya hatari itakayomalizika mwezi Aprili mwakani ni watu wa jamii za Oromia na Amhara.

Zaidi ya watu elfu 11 walikamatwa na kuwekwa korokoroni nchini Ethiopia tangu Oktoba mwaka huu, kwa kukiuka sheria ya hali ya hatari iliyotangazwa nchini humo katika hali ambayo, mivutano ya kisiasa, malalamiko na upinzani wa wananchi ungali unaendelea kushuhudiwa nchini humo.

Makabila mawili ya Oromo na Amhara ambayo yanaunda karibu asilimia 60 ya watu wote wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika yamekuwa yakiituhumu serikali ya Addis Ababa kwamba inatenga na kuyanyanyasa makabila hayo kwa maslahi ya wenzao Watigray ambao wamepewa nyadhifa muhimu serikalini, jeshini na kwenye vyombo vingine vya usalama.