Indhari ya Odinga juu ya kufanyika uchaguzi usio wa kidemokrasia nchini Kenya
(last modified Fri, 23 Dec 2016 16:44:43 GMT )
Dec 23, 2016 16:44 UTC
  • Indhari ya Odinga juu ya kufanyika uchaguzi usio wa kidemokrasia nchini Kenya

Huku vuta nikuvute baina ya serikali na mrengo wa upinzani nchini Kenya kuhusiana na mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 ukiwa unaendelea, kinara wa muungano wa upinzani wa CORD Raila Odinga ametahadharisha tena juu ya kufanyika uchaguzi usio wa kidemokrasia nchini humo.

Sambamba na hayo Odinga ametoa wito wa kufanywa maandamano ya kupinga sheria mpya za uchaguzi zinazoidhinisha kuhesabiwa kura kwa mkono.

Jana Alkhamisi ya tarehe 22 Desemba, Bunge la Kenya lilipitisha sheria mpya za uchaguzi katika mchakato uliosusiwa na wabunge wa mrengo wa upinzani. Kwa mujibu wa sheria hizo, endapo utatokea mushkili katika mfumo wa digitali wa kuhesabu kura, utaratibu wa kuhesabu kura kwa mkono utatumika badala yake.

Mivutano ya kisiasa kuhusiana na jinsi ya kuitisha uchaguzi mkuu unaotazamiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka ujao wa 2017 ilianza kitambo nyuma, na licha ya mazungumzo ya mara kwa mara yaliyofanyika baina ya serikali na muungano wa vyama vya upinzani wa CORD, hitilafu kadhaa bado hazijatatuliwa. Miongoni mwa matakwa ya msingi yaliyokuwa yakipiganiwa na CORD ni kutaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ifanyiwe mabadiliko, baada ya kuituhumu tume hiyo kuwa iliubeba muungano tawala wa Jubilee katika uchaguzi mkuu uliopita. Wakati mchakato wa kuifumua IEBC ukiwa ungali unaendelea, changamoto nyingine imeibuka hivi sasa ambayo ni kupitishwa mabadiliko ya sheria za uchaguzi yaliyopendekezwa na muungano tawala wa Jubilee.

Bunge la Kenya

Wapinzani wanasema mfumo wa kuhesabu kura kwa mkono unatoa mwanya mkubwa wa kufanyika mizengwe na uchakachuaji kura na kubatilisha matokeo halali ya uchaguzi.

Mivutano kuhusiana na mchakato wa uchaguzi nchini Kenya inashuhudiwa katika hali ambayo polisi ya nchi hiyo imekuwa ikiandamawa na lawama kutokana na kutumia ukatili na nguvu kupindukia katika kukabiliana na mikusanyiko na maandamano ya wapinzani. Kutokana na kushtadi malalamiko dhidi ya utendaji wa polisi, mkuu wa jeshi hilo aliamuru ufanyike uchunguzi kamili juu ya suala hilo. Pamoja na hayo mamia ya Wakenya wameanzisha kampeni ya nchi nzima kwa anuani ya "Simamisheni mauaji yanayofanywa na Polisi" kulalamikia vitendo vya ukatili vinavyofanywa na askari polisi dhidi ya wapinzani.

Ukandamizaji wa raia unaofanywa na Polisi

Hii ni katika hali ambayo Rais Uhuru Kenyatta ametangaza kuwa uchaguzi mkuu ujao utafanyika katika anga ya amani. Kenyatta ameahidi pia kwamba uchaguzi huo utakuwa huru na utafanyika kwa uwazi.

Pamoja na hayo ukweli ni kwamba Kenya inakabiliwa na changamoto kadhaa hivi sasa. Kwa upande mmoja hujuma za kigaidi hususan mashambulio ya kundi la kigaidi la Al-Shabaab la Somalia zingali ni tishio kwa usalama wa nchi hiyo. Kuwa jirani na Somalia na uwepo wa wimbi la wakimbizi waliokwenda kutafuta hifadhi nchini Kenya ni changamoto nyingine inayoikabili nchi hiyo. Ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma ni tatizo sugu linaloendelea kuisokota Kenya. Takwimu zinaonyesha kuwa Kenya ni moja ya nchi zenye ufisadi mkubwa zaidi duniani. Licha ya ahadi kubwa kubwa zinazotolewa na viongozi wa nchi hiyo za kupambana na ufisadi na rushwa, hadi sasa hakuna mafanikio ya maana yaliyopatikana. Wananachi wanahisi, serikali bado haijachukua hatua za dhati za kutokomeza vitendo vya ulaji rushwa ulioenea nchini humo.

Rais Uhuru Kenyatta

Hali ya uchumi na migomo ya wafanyakazi wa kada tofauti ni changamoto nyingine inayoikabili serikali ya Rais Kenyatta. Mgomo wa madaktari na wauguzi uliofanyika wiki kadhaa nyuma ulisababisha vifo vya idadi kadhaa ya wagonjwa na kuzusha mtafaruku mkubwa katika sekta ya tiba ya nchi hiyo. Changamoto zote hizo zinaweza kuufanya uchaguzi mkuu ujao ugubikwe na wingu zito la shaka na dhana hasi. Katika hali kama hiyo, uchaguzi ujao na mchakato wa uendeshaji wake ni suala muhimu sana, si kwa Kenya pekee, bali kwa eneo zima la Afrika Mashariki.

Endapo hitilafu zilizopo baina ya muungano tawala wa Jubilee na ule wa upinzani wa CORD hazitoweza kupatiwa ufumbuzi kwenye meza ya mazungumzo, na uchaguzi ukashindwa kufanyika katika anga huru na ya kidemokrasia, matokeo ya hali hiyo yanaweza kuisababishia madhara na matatizo zaidi nchi hiyo…/

 

Tags