Al Shabab yamuua Mwendesha Mashtaka wa Jeshi, Puntland
Kundi la kigaidi la al Shabab limempiga risasi na kumuua Mwendesha Mashtaka wa Jeshi katika eneo lenye mamlaka ya ndani la Puntland nchini Somalia.
Abdikarim Hassan Firdiye alipigwa risasi kichwani jana alipokuwa akiteremka kwenye gari lake nje kidogo ya mgahawa mmoja wa mji mkubwa zaidi wa Puntland, Bosasso.
Siku chache zilizopita pia wanachama wa kundi la al Shabab walimuua kwa kumpiga risasi Naibu wa Mkuu wa kanda hiyo na vilevile Naibu wa Kamanda wa Polisi ya Puntland nje ya mgahawa mmoja.
Ripoti zinasema Mwendesha Mashtaka wa Jeshi katika eneo lenye mamlaka ya ndani la Puntland, Abdikarim Hassan Firdiye amepigwa risasi kichwani na vijana wawili ambao walitoweka haraka baada ya uhalifu huo.
Msemaji wa kundi la kigaidi la al Shabab Abdiasis Abu Musab ametangaza kuwa, kundi hilo limehusika na mauaji hayo na kudai kuwa, Abdikarim Hassan Firdiye aliwahukumu kifo wapiganaji wengi wa al Shabab.