Uchaguzi wa Rais nchini Somalia waakhirishwa kwa mara ya nne
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i22177-uchaguzi_wa_rais_nchini_somalia_waakhirishwa_kwa_mara_ya_nne
Uchaguzi wa Rais nchini Somalia uliokuwa umepangwa kufanyika Jumatano ijayo ya tarehe 28 ya mwezi huu wa Desemba umeakhirishwa tena.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 26, 2016 12:47 UTC
  • Uchaguzi wa Rais nchini Somalia waakhirishwa kwa mara ya nne

Uchaguzi wa Rais nchini Somalia uliokuwa umepangwa kufanyika Jumatano ijayo ya tarehe 28 ya mwezi huu wa Desemba umeakhirishwa tena.

Afisa mmoja wa serikali ya Somalia ambaye hakutaka kutajwa jina lake amesema kuwa, uchaguzi huo umeakhirishwa na kwamba kuna uwezekano tarehe nyingine ya kufanyika uchaguzi ikawa ni 24 Januari mwakani.

Hii ni mara ya nne kwa uchaguzi wa Rais nchini Somalia kuakhirishwa kwa sababu mbalimbali zikiwemo za ukosefu wa usalama.

Mwanzoni mwa mwezi huu viongozi wa kisiasa Somalia waliafikiana kuwa uchaguzi wa rais ufanyike Desemba 28 ambapo ilitarajiwa kwanza bunge jipya limchague spika tarehe 22 Disemba ambaye baada ya hapo asimamie zoezi la wabunge kumchagua rais.

Wanamgambo wa al-Shabab wa Somalia

Uchaguzi wa Bunge ulifanyika kama ilivyokuwa imepangwa; na Wabunge hao Jumatano ya wiki hii wataapishwa tayari kwa ajili ya kuanza duru nyingine ya Bunge la nchi hiyo iliyoko katika eneo la Pembe ya Afrika.

Kwa mujibu wa Katiba ya Somalia, Rais wa nchi hachaguliwi moja kwa moja kwa kura za wananchi bali huchaguliwa na wawakilishi wa Bunge.

Viongozi wa upinzani nchini Somalia wameelezea wasiwasi walionao kutokana na kuakhirishwa tena zoezi la kumchagua Rais wa nchi hiyo.

Somalia ambayo inafanya juhudi za kukarabati uharibifu wa miongo kadhaa iliyopita, inakabiliwa na mashambulizi ya wanamgambo wa kundi hatari la kigaidi na kitakfiri la ash-Shabab.