Mtu anayedai kiongozi wa Boko Haram akanusha kutekwa kambi ya Sambisa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i22411-mtu_anayedai_kiongozi_wa_boko_haram_akanusha_kutekwa_kambi_ya_sambisa
Mtu aliyejitambulisha kuwa ni Abubakar Shekau, kiongozi wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram la nchini Nigeria amekanusha kuwa kundi hilo limefurushwa kwenye ngome yake kuu iliyoko kwenye msitu wa Sambisa kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 30, 2016 07:12 UTC
  • Mtu anayedai kiongozi wa Boko Haram akanusha kutekwa kambi ya Sambisa

Mtu aliyejitambulisha kuwa ni Abubakar Shekau, kiongozi wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram la nchini Nigeria amekanusha kuwa kundi hilo limefurushwa kwenye ngome yake kuu iliyoko kwenye msitu wa Sambisa kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Akizungumza kwa lugha ya Kihausa na Kiarabu kupitia mkanda wa video uliosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, mtu huyo aliyejitambulisha kuwa ni Abubakar Shekau amesema: "Tuko salama. Hatujatimuliwa popote pale". "Kama ni kweli mumetusambaratisha, vipi mnaweza kuniona mimi kama hivi?" ameendelea kueleza mtu huyo anayedai kuwa kiongozi wa Boko Haram.

Hata hivyo msemaji wa jeshi la Nigeria Sani Usman ameyapuuza madai hayo na kutilia mkazo kauli ya awali ya jeshi hilo kuwa limeiteka kambi hiyo kuu ya kundi la Boko Haram na kuwasambaratisha wanamgambo wa kundi hilo la kigaidi.

"Jeshi la Nigeria lingependa kusisitiza kuwa limeiteka na kuidhibiti ngome kuu ya mwisho inayojulikana ya kundi la kigaidi katika msitu wa Sambisa", ameeleza Usman.

Askari wa Jeshi la Nigeria

Matamshi ya mtu aliyejitambulisha kuwa Abubakar Shekau yametolewa katika hali ambayo jeshi la Nigeria limeshawahi kutangaza mara kadhaa katika miaka ya karibuni kuwa limemuua au kumjeruhi kiongozi huyo wa Boko Haram, lakini baadaye amekuwa akijitokeza kupitia mikanda ya video na kukanusha madai hayo.

Itakumbukwa kuwa hivi karibuni Rais Muhammad Buhari wa Nigeria alitangaza kuwa jeshi la nchi hiyo limeiteka ngome kuu ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram katika msitu wa Sambisa.

Magaidi wa kundi la kitakfiri la Boko Haram

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram limeua watu wasiopungua 15,000 katika uasi na mashambulio yake liliyoanzisha miaka saba nyuma na kuwafanya wengine zaidi ya milioni mbili wabaki bila ya makaazi.

Kundi hilo lilikuwa limedhibiti sehemu kubwa ya eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria, lakini tangu mapema mwaka jana limetimuliwa kwenye karibu maeneo yote na jeshi la serikali likisaidiwa na vikosi vya mataifa jirani.../