Makundi ya kisiasa Kongo yafikia muafaka wa kuhitimisha mgogoro nchini humo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i22498-makundi_ya_kisiasa_kongo_yafikia_muafaka_wa_kuhitimisha_mgogoro_nchini_humo
Imetangazwa kuwa Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo atang'atuka madarakani kabla ya kufanyika uchaguzi ujao hiyo ikiwa ni baada ya kufikiwa muafaka wa kisiasa kwa ajili ya kuhitimisha mgogoro wa kisiasa nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 31, 2016 13:01 UTC
  • Makundi ya kisiasa Kongo yafikia muafaka wa kuhitimisha mgogoro nchini humo

Imetangazwa kuwa Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo atang'atuka madarakani kabla ya kufanyika uchaguzi ujao hiyo ikiwa ni baada ya kufikiwa muafaka wa kisiasa kwa ajili ya kuhitimisha mgogoro wa kisiasa nchini humo.

Marcel Utembi Mpatanishi wa ngazi ya juu wa Kanisa Katoliki nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amethibitisha suala hilo na kuongeza kuwa, kwa mujibu wa muafaka uliofikiwa kati ya makundi ya kisasa ya nchi hiyo, Rais Joseph Kabila atang'atuka madarakani kabla ya kufanyika chaguzi za rais na bunge mwezi Disemba mwakani. 

Mkuu wa Umoja wa Maaskofu wa Kikatoliki nchini Kongo ameeleza kuwa, kwa mujibu wa muafaka uliofikiwa, Kabila hatoweza kuifanyia marekebisho katiba ya Kongo ili agombee tena urais kwa muhula wa tatu. Kanisa Katoliki nchini Kongo ambalo limechukua nafasi ya usuluhishi kati ya serikali na upinzani limetoa hakikisho kuwa, vizuizi vyote kwa ajili ya kusaini makubaliano ya kuiondoa Kongo katika hali ya mgogoro uliosababishwa na hatua ya Rais Kabila ya kutaka kusalia madarakani vimeondolewa.

Wawakilishi wa mazungumzo ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa wa Kongo 

Mgogoro wa kisiasa ulipamba moto huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufuatia kuakhirishwa tarehe ya uchaguzi wa rais na pia kuendelea kusisitiza Joseph Kabila kubakia uongozini. Joseph Kabila ambaye aliingia madarakani mwaka 2001 baada ya kuuliwa baba yake Laurent Kabila, alishinda chaguzi mbili za rais zilizofanyika mwaka 2006 na 2011. Hata hivyo kwa mujibu wa katiba ya Kongo, Kabila hawezi kugombea kiti cha urais kwa muhula wa tatu. Wapinzani wanasema kuwa Kabila ana lengo la kusalia madarakani sawa kabisa na wanavyofanya baadhi ya viongozi wa nchi za Kiafrika. Wapinzani hao waliamini kuwa kuakhirisha uchaguzi kungempa  Kabila fursa ya kuifanyia marekebisho katiba  na hivyo kuendelea kubaki katika hatamu za uongozi. Aidha baadhi ya makundi ya upinzani huko Kongo yanaamini kuwa kuakhirishwa uchaguzi  kunakipatia muda unaohitajika chama tawala kwa ajili ya kupanga na kuiba kura katika uchaguzi. Katika hali ambayo makundi ya upinzani yanakosoa vikali hali hiyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Kongo  imetangaza kuwa uchaguzi umeakhhirishwa nchini humo kutokana na kukosekana suhula hitajika kwa ajili ya kuendeshea uchaguzi kama vile uhaba wa bajeti na kadhalika. Suala hilo lilipelekea kuibuka machafuko ya kisiasa kati ya wapinzani na askari usalama wa nchi hiyo; makabiliano ambayo yalisababisha kuuliwa na kujeruhiwa wafuasi wengi wa upinzani. Maandamano ya wafuasi wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ya kumtaka Rais Kabila ang'atuke madarakani baada ya muhula wake kumalizika mwezi huu wa Disemba, yalisababisha vifo vya watu wasiopungua 27 na wengine zaidi ya 270 kutiwa mbaroni. 

Maandamano ya wafuasi wa upinzani Kinshasa dhidi ya Rais Kabila 

Hata kama mchakato huo wa kisiasa ulikabiliwa na malalamiko ya viongozi wa ndani ya Kongo kwenyewe na kieneo  na pia viongozi wengi wa kimataifa akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kutaka kukomeshwa ghasia huko Kongo na kutekelezwa sheria, lakini licha ya upinzani huo wote, Kabila alitangaza kuwa, ataendelea kuwepo madarakani hadi kutakapofanyika uchaguzi ujao mwaka 2018 kwa mujibu wa kibali cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo. Hata hivyo hivi sasa inatazamiwa kuwa Kabila atabaki madarakani kwa mwaka mmoja mwingine hadi 2017 na baada ya hapo itaundwa serikali itakayowajumuisha wawakilishi wa serikali na wa upande wa upinzani na baadaye kuzindua mchakato wa maandalizi ya uchaguzi . Kwa msingi huo, muafaka uliofikiwa kati ya serikali na upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unaweza kuwa mwanzo wa kuhitimishwa mgogoro wa kisiasa nchini humo, mgogoro ambao iwapo hautahitimishwa, unaweza kupelekea kuibuka vita vya ndani nchini humo.