Jan 07, 2017 15:56 UTC
  • Kundi la Niger Delta latangaza rasmi vita na serikali ya Nigeria

Kundi la waasi wa Niger Delta kusini mwa Nigeria limetangaza vita na serikali ya nchi hiyo kufuatia kushindwa mazungumzo ya pande mbili.

Taarifa iliyotolewa na kundi hilo imesema kuwa, kitendo cha serikali ya Abuja cha kutokuwa na azma ya kufanya mazungumzo, ndicho kilicholifanya kundi hilo la waasi kutangaza vita. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wapiganaji na makamanda wote wa kundi la Niger Delta sasa wanatakiwa kujiweka tayari kikamilifu kwa ajili ya kupambana na serikali.

Waasi wa kundi la Niger Delta

Itafahamika kuwa, mwaka jana kundi hilo na baada ya kufanya mashambulizi mengi dhidi ya taasisi za mafuta nchini Nigeria ambayo ni mwanachama wa Jumuiya ya Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa Wingi Duniani OPEC, liliamua kutangaza usitishaji vita kama fursa ya kuanza mazungumzo na viongozi wa serikali ya Abuja juu ya ugawanaji pato litokanalo na nishati hiyo muhimu.

Baada ya hatua hiyo, viongozi wa serikali walianzisha mchakato wa mazungumzo na wakuu wa genge hilo la waasi la kusini mwa Nigeria, hata hivyo kutokana na mazungumzo hayo kwenda mwendo wa kinyonga na kutofikiwa natija iliyotarajiwa, kundi hilo limeandika kujitoa kwenye mazungumzo na kutangaza vita dhidi ya serikali.

Tags