Mahakama kusikiliza ombi la Jammeh, Ecowas kurejea Gambia kesho
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i23194-mahakama_kusikiliza_ombi_la_jammeh_ecowas_kurejea_gambia_kesho
Mahakama ya Kilele ya Gambia inatazamiwa hii leo kuanza kusikiliza kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais iliyowasilishwa na Rais Yahya Jammeh anayetaka matokeo ya uchaguzi yabatilishwe.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 10, 2017 08:16 UTC
  • Mahakama kusikiliza ombi la Jammeh, Ecowas kurejea Gambia kesho

Mahakama ya Kilele ya Gambia inatazamiwa hii leo kuanza kusikiliza kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais iliyowasilishwa na Rais Yahya Jammeh anayetaka matokeo ya uchaguzi yabatilishwe.

Awali mahakama hiyo ambayo mwenyekiti wake ni Jaji Mkuu Emmanuel Fagbenle iliamuru kesi hiyo iakhirishwe kwa sababu Tume Huru ya Uchaguzi Gambia ilikuwa bado haijapokea nyaraka za kesi. Hii ni katika hali ambayo, Alieu Momar Njai, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi Gambia alikimbia nchi baada ya kutishiwa maisha kwa kumtangaza Adama Barrow mshindi wa uchaguzi wa Disemba Mosi mwaka uliomalizika 2016.  

Rais Jammeh ameyakataa matokeo ya uchaguzi wa rais kwa madai ya kile alichokiita makosa yasiyokubalika yaliyofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Gambia na kutaka uitishwe uchaguzi mwingine mpya.

Adama Barrow, Rais mteule wa Gambia

Katika hali ambayo taharuki imetanda nchini humo huku kesi hiyo ikisubiriwa kwa hamu na shauku kuu, maafisa usalama hususan wanajeshi waliotangaza utiifu wao kwa Jammeh wameonekana wakishika doria katika kila kona ya mji mkuu, Banjul. 

Huku hayo yakiarifiwa, viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika wanatazamiwa kusafiri kuelekea Gambia kesho Jumatano, katika kile kinachotajwa kuwa safari ya mwisho ya kujaribu kumshawishi Jammeh kuachia ngazi na kumkabidhi madaraka Rais mteule Adama Barrow.

Mapema mwezi huu, Jammeh aliitumu ECOWAS kuwa imemtangazia vita baada ya jumuiya hiyo kusema kuwa inaviweka vikosi vyake ya jeshi katika hali ya tahadhari endapo kiongozi huyo atakataa kuondoka madarakani baada ya muhula wake wa uongozi kumalizika tarehe 19 mwezi huu wa Januari

Marais na viongozi wa Ecowas