Dakta Shein amjibu Maalim Seif, asema madai yake ni ya kipropaganda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i23197-dakta_shein_amjibu_maalim_seif_asema_madai_yake_ni_ya_kipropaganda
Rais wa Zanzibar Dakta Ali Mohamed Shein amewataka wananchi visiwani humo kuacha kusikiliza kile alichokitaja kuwa maneno ya propaganda kutoka kwa wapinzani kwa kuwa katu hakuna Rais mwingine atakayeongoza Zanzibar wakati yeye yupo madarakani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 10, 2017 04:48 UTC
  • Dakta Shein amjibu Maalim Seif, asema madai yake ni ya kipropaganda

Rais wa Zanzibar Dakta Ali Mohamed Shein amewataka wananchi visiwani humo kuacha kusikiliza kile alichokitaja kuwa maneno ya propaganda kutoka kwa wapinzani kwa kuwa katu hakuna Rais mwingine atakayeongoza Zanzibar wakati yeye yupo madarakani.

Shein alisema hayo jana baada ya kuzindua soko na ofisi ya Baraza la Mji la Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, ikiwa ni sehemu ya sherehe za miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Gazeti la Mwananchi la Tanzania limemnukuu Rais Shein akisema kuwa, kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wakipita mitaani na kujinadi kwa wananchi kuwa huenda wakawa marais wakati wowote, huku wakimkataa yeye kuwa si Rais halali wa Zanzibar.

Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar

Ingawaje Dakta Shein hakutaja jina, lakini Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ndiye ambaye amekuwa akitoa kauli za namna hiyo za kupinga uhalali wa Shein kuwa madarakani.

Siku chache zilizopita akihutubia mkutano wa kampeni alisema, “Hata wafanye kitu gani mwaka huu msumari umewaganda na hivi karibuni Wazanzibari watafurahia mambo yao mazuri.”

Maalim Seif ambaye alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais visiwani humo amesema mipango imara ya kuhakikisha kuwa mambo hayo yanakaa sawa inakwenda vizuri na wakati wowote matunda hayo yataonekana.

Shein na Maalim Seif kabla ya kuwa mahasimu wa kisiasa

Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC ilimtangaza mgombea wa kiti cha rais kupitia Chama cha Mapinduzi CCM, Dakta Ali Muhammed Shein kuwa mshindi wa uchaguzi wa marudio uliofanyika mwezi Machi mwaka jana visiwani humo.