Waziri wa Gambia aihama serikali ya Rais Jammeh
Waziri wa Mawasiliano wa Gambia Sheriff Bojang amesema ameamua kujiondoa kwenye serikali tangu rais Yahya Jammeh wa nchi hiyo alipokataa kuwa ameshindwa katika uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe mosi ya mwezi uliopita wa Desemba.
Katika taarifa aliyoisambaza kwa vyombo vya habari, waziri huyo ameielezea hatua ya Jammeh kuwa ni jaribio la kupindua matakwa ya wapiga kura wa Gambia.
"Gambia imeamua na tunapaswa kukubali na kuheshimu uamuzi huu", amesema Bojang, akinukuu bango maarufu ambalo lilikuwepo katika mji mkuu Banjul na kuondolewa na askari wa serikali katika wiki za hivi karibuni.
Waziri wa Mawasiliano wa Gambia aidha ametoa wito kwa mawaziri wengine kuungana naye katika uamuzi aliochukua.
Wapinzani wa Rais Jammeh wana matumaini kwamba uamuzi wa waziri huyo unaweza kupelekea kiongozi huyo kuachwa mkono na waitifaki wake wengine wa ndani ya nchi wanaoendelea kudhibiti jeshi na vyombo vingine vya dola.
Waziri wa Mambo ya Nje Neneh Macdouall Gaye alijiuzulu wadhifa wake mwezi Desemba, japokuwa hatua yake hiyo haikutoa mguso mkubwa kwa hisia za wananchi.
Rais Yahya Jammeh ambaye alikuwa amekubali kushindwa na mpinzani wake Adama Barrow katika uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi Desemba na hata kuchukua hatua ya kumpongeza mpinzani wake, alibadilisha uamuzi na kuyakataa matokeo kwa madai kuwa zoezi la uchaguzi lilitawaliwa na dosari nyingi na anataka uchaguzi wa rais ufanyike tena.
Maafisa wengi na wafanyabiashara wameitoroka nchi kwa hofu ya kuandamwa na mkono wa chuma wa luteni huyo wa zamani wa jeshi ambaye alitwaa madaraka ya nchi akiwa na umri wa miaka 29 katika mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika mwaka 1994. Jammeh anatuhumiwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu kuwa anawafunga jela kiholela na hata kuwaua wakosoaji wake…/