Mahakama Kuu ya Gambia yakataa kusikiliza shauri la malalamiko ya uchaguzi
Mahakama Kuu ya Gambia imetangaza kuwa katika hali ya sasa haiwezi kusikiliza na kutoa uamuzi kuhusu malalamiko ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais wa nchi hiyo.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Gambia, Emmanuel Fagbenle, ametangaza kuwa kutokana na kutokuwa na majaji, mahakama hiyo haiko katika mazingira ya kuweza kutoa uamuzi kuhusu malalamiko yaliyowasilishwa na Rais Yahya Jammeh, mgombea urais aliyeshindwa katika uchaguzi huo.
Fagbenle, amesema mahakama hiyo itatoa uamuzi wake kuhusiana na kesi hiyo ya uchaguzi baada ya idadi ya jopo la majaji la kusikiliza shauri hilo itakapokamilika.
Rais Yahya Jammeh ambaye alikuwa amekubali kushindwa na mpinzani wake Adama Barrow katika uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi Desemba na hata kuchukua hatua ya kumpongeza mpinzani wake, alibadilisha uamuzi na kuyakataa matokeo kwa madai kuwa zoezi la uchaguzi lilitawaliwa na dosari nyingi na sasa anataka uchaguzi wa rais ufanyike tena.
Juhudi za viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Uchumi wa Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) za kumshawishi Rais huyo wa Gambia akubali kungátuka madarakani, hadi sasa zimeshindwa kuzaa matunda.../