UNOWAS kuhakikisha Jammeh anaondoka madarakani nchini Gambia
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa Afrika Magharibi amesema kunafanyika jitihada za kumshawishi Yahya Jammeh aliyeshindwa katika uchaguzi wa rais Gambia kuondoka madarakani na kumuachia mshindi, Adama Barrow, achukue hatamu za uongozi nchini humo.
Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa ofisi ya umoja huo ukanda wa Afrika Magharibi UNOWAS, Mohamed Ibn Chambas aliyasema hayo Ijumaa katika kikao cha Baraza la Usalama la umoja huo mjini New York.
Wajumbe wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa walikuwa wamekutana ili kupokea taarifa kuhusu hali ya usalama na kibinadamu huko Afrika Magharibi na kushauriana kuhusu ukanda huo, ambapo wameelezwa kuwa juhudi zinaendelea ili kuhakikisha Rais wa Gambia aliyeshindwa uchaguzi hivi karibuni anaachia madaraka.
Ibn Chambas amelimbia baraza hilo kuwa UNOWAS inatambua na kuzingatia majadiliano yanaoongozwa na jumuiya ya kiuchumi Afrika Magharibu ECOWAS katika kuhakikisha Rais liyeshindwa Yahya Jammeh anaachia madaraka na hivyo kuruhusu Rais mteule Adam Barrow kuapishwa.
Amesema ujumbe wa ngazi ya juu wa ECOWAS ulirejea mjini Banjul Januari 13 katika majaribio ya kumshawishi Rais Jammeh akubali matokeo ya uchaguzi na kuondoka madarakani.''
Amesema ikiwa ushawishi utashindikana kuna mpango wa kuutumia kila mbinu ikiwemo ya matumizi ya nguvu kuhakikisha matakwa ya watu wa Gambia yanatimizwa. Amesema ikiwa kutahitajika nguvu za kijeshi kumuondoa Jammeh, ECOWAS inatarajia kusaka ridhaa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika ili kutuma vikosi Gambia.'
Rais Yahya Jammeh ambaye alikuwa amekubali kushindwa na Adama Barrow katika uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi Desemba na hata kumpongeza mpinzani wake, ghafla alibadilisha uamuzi na kuyakataa matokeo hayo kwa madai kuwa zoezi la uchaguzi lilitawaliwa na dosari nyingi na sasa anataka uchaguzi wa rais ufanyike tena.