Raia waliotekwa nyara na waasi wa Uganda Kongo DR wakombolewa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i24141-raia_waliotekwa_nyara_na_waasi_wa_uganda_kongo_dr_wakombolewa
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limefanikiwa kuwakomboa raia kadhaa waliokuwa wanashikiliwa na waasi wa Uganda huko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 23, 2017 23:27 UTC
  • Raia waliotekwa nyara na waasi wa Uganda Kongo DR wakombolewa

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limefanikiwa kuwakomboa raia kadhaa waliokuwa wanashikiliwa na waasi wa Uganda huko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Carlos Kalombo, kamanda wa jeshi la nchi hiyo amesema kuwa, askari wa serikali ya Kinshasa wamefanikiwa kuwakomboa  raia 17 wa nchi hiyo kutoka mikononi mwa waasi wa uganda. Kwa mujibu wa Kalombo, raia hao wamekombolewa wakiwa salama baada ya kujiri mapigano makali na waasi hao katika eneo la Dungu la mkoa wa Haut-Ulele, kaskazini mashariki mwa Kongo. Sambamba na kuashiria kuwa raia hao walikuwa mikononi mwa waasi kwa kipindi cha siku tatu amesema kuwa, jeshi la nchi hiyo linaendelea na operesheni kali ya kuwakomboa raia wengine ambao bado wako mikononi mwa waasi hao wa Uganda ambao wanaendesha harakati za uasi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Waasi wa Uganda wanaoharibu usalama wa Kongo DR

Raia hao wapatao 25 walitekwa nyara siku tatu zilizopita katika kijiji cha Nango, kilichopo eneo la Dungu mkoani Haut-Uele, kaskazi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa Kongo DR yamekuwa yakishuhudia hali ya mchafukoge kwa miaka 20 sasa, kutokana na udhaifu wa askari wa serikali na wale wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa.