Morocco kujua iwapo itarejea AU, wananchi waandamana dhidi ya serikali
Katika hali ambayo Morocco inasubiri kujua iwapo ombi lake la kutaka kurejea katika Umoja wa Afrika litapata uungaji mkono au la katika mkutano wa AU huko Addis Ababa, wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu wamefanya maandamano wakilalamikia ufisadi wa serikali.
Mwanadiplomasia wa ngazi za juu wa Morocco ambaye hakutaka kutajwa jina amewaambia waandishi wa habari mjini Addis Ababa kuwa, nchi hiyo itapata uungaji mkono wa kishindo wa kurejea Umoja wa Afrika akifafanua kuwa, tayari wamepata uungaji mkono wa nchi 42 kati ya 54 wanachama wa AU.
Mkutano wa nchi wanachama wa AU unaanza rasmi leo katika makao makuu ya umoja huo mjini Addis Ababa, Ethiopia, ajenda kuu ikiwa ni kadhia ya Morocco na pia kumchagua mwenyekiti mpya wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, ambayo imeongozwa kwa muda na Nkosazana Dlamini-Zuma.
Bunge la Morocco siku chache zilizopita lilipasisha muswada wa kutaka nchi hiyo irejee katika Umoja wa Afrika, miezi kadhaa baada ya Mfalme Mohammed wa VI wa nchi hiyo kutangaza wazi azma ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ya kutaka kurejea AU, baada ya kuondoka katika umoja huo zaidi ya miongo mitatu iliyopita.
Hii ni katika hali ambayo, maelfu ya Wamorocco jana Jumapili walifanya maandamanop katika mji mkuu Rabat, kukosoa ufisadi wa serikali na hatua ya bunge kupasisha dikrii ya kuondolewa ruzuku kwa wafanyakazi wa umma.
Baadhi ya waandamanaji hao aghalabu yao wakiwa ni wanachama wa Chama cha Wafanyakazi cha UMT, walisikika wakipiga nara za "Uhuru! Hadhi! Usawa wa Kijamii!", kaulimbiu iliyotumiwa na waandamanaji wapenda mageuzi wa harakati ya Febuari 20, iliyozaliwa wakati wa wimbi la maandamano dhidi ya serikali katika nchi za Kiarabu mwaka 2011.