Morocco yarejea Umoja wa Afrika baada ya miaka 33
Umoja wa Afrika AU umekubali tena uanachama wa Morocco baada ya miaka 33 wakati nchi hiyo ilijiondoa umoja huo kutokana na mgogoro wa Sahara Magharibi ambao hadi sasa haujatatuliwa.
Aghalabu ya wanachama wa AU wamepiga kura kuiruhusu Morocco kujiunga tena katika mkutano wa 28 wa viongozi wa umoja huo wakati wa mkutano wa kilele uliofanyika Jumatatu katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa. Hata hivyo nchi hizo za Afrika hazikujadili kadhia ya Sahara Maghharibi ambayo ilipelekea Morocco kujiondoa katika umoja huo.
Algeria na Afrika Kusini ni kati ya nchi kubwa Afrika ambazo zilikuwa zinapinga uanachama wa Morocco lakini hazikufanikiwa kwani nchi 39 kati ya 54 zilipiga kura ya kuiruhusu Morocco irejee.

Mwaka 1984 Morocco ilijiondoa katika Umoja wa Afrika AU, wakati huo ukijulikana kama OAU, baada ya eneo la Sahara Magharibi kukubaliwa kama mwanachama wa umoja huo.
Morocco ilichukua udhibiti wa Sahara Magharibi kutoka mkoloni Mhispania mwaka 1975 na inasisitiza kuwa eneo hilo ni sehemu ya ardhi yake. Hata hivyo aghalabu ya nchi duniani zinapinga hatua hiyo ya Morocco.