Somalia na uchaguzi ulioko mbele yake
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i24527-somalia_na_uchaguzi_ulioko_mbele_yake
Baada ya tarehe 8 Februari kutangazwa kuwa ndio siku ya kufanyika uchaguzi wa Rais nchini Somalia, Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo imetangaza kuwa, watu 24 watachuana kuwania kiti hicho cha urais.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 01, 2017 00:50 UTC
  • Somalia na uchaguzi ulioko mbele yake

Baada ya tarehe 8 Februari kutangazwa kuwa ndio siku ya kufanyika uchaguzi wa Rais nchini Somalia, Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo imetangaza kuwa, watu 24 watachuana kuwania kiti hicho cha urais.

Tume hiyo ya uchaguzi inayoundwa na wajumbe 18 ambao ni wabunge imetoa taarifa mjini Mogadishu kwamba, imepasisha majina ya wagombea 24 waliotimiza masharti kwa ajili ya kuchuana katika kinyang'anyiro cha urais  katika uchaguzi ambao umepangwa kufanyika tarehe 8 ya mwezi huu wa Februari.

Waziri Mkuu Abdirashid Ali Shermarke 

Pamoja na kuweko mlolongo wa majina ya wagombea waliojitokeza kuwania kiti cha urais nchini Somalia lakini Rais Hassan Sheikh Mohamud, Waziri Mkuu Abdirashid Ali Shermarke na  Sharif Sheikh Ahmed Rais wa zamani wa Somalia ni miongoni mwa wagombea muhimu wa kinyang'anyiro hicho.

Aidha Mohamed Abdullahi Farmajoo, Waziri Mkuu wa zamani, Muhammad Ali Nur balozi wa zamani wa Somalia nchini Kenya, na Muhammad Ahmed Nor Tarsan meya wa zamani wa Mogadishu ni miongoni mwa wagombea wengine wa kiti cha urais ambao wametimiza masharti. Kwa mujibu wa katiba ya Somalia, kila mgombea anapaswa kutumia kiasi kisichozidi dola elfu thelathini kama gharama zake za uchaguzi.

Hadi sasa uchaguzi wa Rais nchini Somalia umeakhirishwa mara tano. Hivi sasa viongozi wa nchi hiyo wanataraji kwamba, watafanikiwa kufanya uchaguzi huo kwa mafanikio tarehe 8 mwezi huu kama ilivyopangwa. Ikiwa ni katika maandalizi ya uchaguzi huo, Tume ya Uchaguzi ya Somalia imeandaa mdahalo wa wazi kwa wagombea wa kiti hicho cha urais. Katika mdahalo huo utakaorushwa hewani moja kwa moja na televisheni, wagombea hao watatumia fursa hiyo kutangaza sera zao na kutafuta kura na uungaji mkono. Kutokana na sababu za kiusalama,  rais wa Somalia hatochaguliwa moja kwa moja na kura za wananchi, bali Wabunge ndio watakaomchagua kiongozi huyo wa nchi kwa ajili ya kuongoza duru ya miaka minne.

Wanamgambo wa al-Shabab

Ni kwa miaka kadhaa sasa Somalia imekuwa ikikabiliwa na tatizo la ukosefu wa usaalama na uthabiti. Harakati za kundi la al-Shabab na mashambulio ya kundi hilo katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo yamepelekea makumi ya raia wa nchi hiyo kuuawa. Hata kama uwepo wa kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM na ushirikiano wake na jeshi la nchi hiyo kwa namna fulani umezuia kusonga mbele wanamgambo wa al-Shabab katika nchi hiyo na katika eneo, lakini harakati za wanamgambo hao wa kitakfiri zingali zinashuhudiwa.

Katika upande mwingine, gharama za kudhamini mahitaji askari wa kusimamia amani na kuibuka mivutano ya kisiasa baina ya nchi za eneo sambamba na hatua ya Umoja wa Ulaya ya kupunguza bajeti yake ya kusaidia kikosi hicho, ni mambo ambayo yamepelekea askari hao wa kusimamia amani wakumbwe na changamoto kubwa. Hitilafu na mizozo hiyo imepelekea Burundi itangaze kwamba itaondoa askari wake kutoka Somalia.

Mbali na suala la ugaidi na ukosefu wa usalama, tatizo la uchumi na ukame mkubwa unaoyakabili maeneo mengi ya nchi hiyo ni changamoto nyingine kubwa inayoikabili Somalia. Filihali, sehemu kubwa ya Somalia inakabiliwa na ukame mkubwa.

Mohamed Siad Barre, Rais wa zamani wa Somalia ambaye utawala wake uliangushwa mwaka 1991

Suala la kudhamini bidhaa za chakula ndio daghadagha kuu ya wakazi wa nchi hiyo. Katika upande mwingine, kuongezeka umasikini na ukosefu wa ajira hususan miongoni mwa vijana wa Somalia ni mambo ambayo yameifanya nchi hiyo izidi kukabiliwa na ukosefu wa usalama kuliko huko nyuma. Kutokana na hali hiyo akthari ya vijana wa Somalia wamekuwa wakijunga na makundi ya kigaidi au na maharamia. Hivi sasa ukanda wa maji ya Somalia umegeuka na kuwa moja ya maeneo makuu ya harakati za maharamia ulimwenguni.

Katika mazingira kama haya, inaonekana kuwa, kufanyika uchaguzi wa rais nchini Somalia ni kibarua kigumu na cha aina yake. Pamoja na hayo, viongozi wa Somalia na maafisa wa asasi za kimataifa wanaamini kwamba, kufanyika uchaguzi huo kutakuwa ni hatua muhimu katika njia ya kuboresha hali ya mambo nchini humo.

Milipuko ya mara kwa mara hutokea Somalia

Ikiwa uchaguzi huo utafanyika kwa mafanikio, basi kwa mara nyingine tena wananchi wa nchi hiyo watanufaika na uwepo wa serikali kuu ikiwa ni miaka zaidi ya ishirini tangu ulipoangushwa utawala wa Mohamed Siad Barre.