Al Shabab washambulia kusini mwa Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i24555-al_shabab_washambulia_kusini_mwa_somalia
Watu wawili wameripotiwa kuuawa baada ya kundi la kigaidi la al Shabab kufanya shambulio kusini mwa Somalia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 01, 2017 12:12 UTC
  • Al Shabab washambulia kusini mwa Somalia

Watu wawili wameripotiwa kuuawa baada ya kundi la kigaidi la al Shabab kufanya shambulio kusini mwa Somalia.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Abdi Bareh, mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa Somalia akitangaza habari hiyo leo na kusema kuwa, wanamgambo wa al Shabab wameshambulia kambi moja ya kijeshi ya Somalia katika mji wa Hudur, kusini mwa nchi hiyo na kuua wajeshi wasiopungua wawili na kujeruhi wengine kadhaa.

Amesema, hivi sasa kundi la al Shabab limeamua kufanya mashambulizi ya kushtukiza dhidi ya maeneo ya kijeshi nchini humo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, juhudi za askari wa Somalia za kuchunguza kwa kina za kugundua mazingira ya shambulio hilo, zingali zinaendelea.

Askari wa AMISOM wakiwa kwenye operesheni maalumu nchini Somalia

 

Hivi sasa kuna wanajeshi elfu 22 wa Umoja wa Afrika wanaojulikana kwa jina la AMISOM, wanashirikiana na askari wa Somalia kupambana na kundi la kigaidi la al Shabab. Wanajeshi hao wa AMISOM ni kutoka nchi za Uganda, Kenya, Burundi, Ethiopia ambao wanashirikiana na polisi kutoka Nigeria na Sierra Leone kuendesha operesheni za AMISOM nchini Somalia.

Ikumbukwe kuwa, mwaka 2012, kundi la kigaidi la al Shabab lilitangaza rasmi kuwa ni sehemu ya makundi ya mtandao wa kigaidi wa al Qaida.

Katika miaka ya huko nyuma, kundi hilo lilifanikiwa kuteka maeneo mengi ya kusini na kaskazini mwa Somalia. Hata hivyo mwaka 2015 lilipoteza miji yote mikubwa na hivi sasa liko katika maeneo madogomadogo tu ya vijijini. Pamoja na hayo huwa linafanya mashambulizi ya mara kwa mara ya kuvizia.