Mfalme wa Morocco aitembelea Sudan Kusini
Mfalme Mohammed wa VI wa Morocco yuko nchini Sudan Kusini katika ziara ya siku tatu iliyoanza jana Jumatano, siku moja baada ya nchi hiyo kurejea katika Umoja wa Afrika.
Ziara hiyo inaonekana kuwa ni ya kujaribu kuimarisha ushawishi wa Morocco katika masuala ya uwekezaji na diplomasia kati ya Rabat na nchi za bara Afrika, baada ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika kukubaliwa tena AU.
Mbali na kusaini makubaliano ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili wa Rabat na Juba, Mfamle huyo anatazamiwa kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Salva Kiir kuhusu utekelezaji wa makubaliano ya amani.
Aidha Mfalme Mohammed wa VI wa Morocco leo Alkhamisi anatazamiwa kulihutubia taifa hilo ambalo linakabiliwa na mapigano kati ya vikosi vya serikali na wapinzani kwa muda mrefu sasa.
Mwishoni mwa mwaka uliopita, Mfalme wa Morocco alizitembelea nchi za mashariki na magharibi mwa Afrika, ambapo mbali na kutafuta uungwaji mkono wa kurejea AU, alisaini makubaliano ya ushirikiano na nchi hizo katika nyuga za viwanda, benki, ujenzi, uchimbaji madini na bima.
Jumanne iliyopita, Umoja wa Afrika ulikubali tena uanachama wa Morocco baada ya miaka 33 wakati nchi hiyo ilijiondoa umoja huo kutokana na mgogoro wa Sahara Magharibi ambao hadi sasa haujatatuliwa.
Mwaka 1984 Morocco ilijiondoa katika Umoja wa Afrika AU, wakati huo ukijulikana kama OAU, baada ya eneo la Sahara Magharibi kukubaliwa kama mwanachama wa umoja huo. Morocco inaihesabu jamhuri hiyo kuwa ni sehemu ya ardhi yake.