Misri na Cameroon kumenyana katika fainali ya kombe la mataifa ya Afrika
Timu ya taifa ya soka ya Cameroon imeitandika Ghana mabao mawili kwa nunge katika mchezo wa nusu fainali wa kombe la Mataifa ya Afrika na hivyo kujikatia tiketi ya kucheza fainali ya mashindano hayo yanayofanyika nchini Gabon.
Mabao yaliyoipaisha Cameroon hadi fainali yalipachikwa wavuni katika kipindi cha pili. Bao la kwanza liliwekwa kimiani na Michael Ngadeu-Ngadjui katika dakika ya 72. Huku timu ya taifa ya soka ya Ghana ikiwa katika juhudi za kutaka kusawazisha, ilijikuta ikifungwa bao la pili katika dakika ya 90 ya mchezo na mchezaji hatari wa Cameroon Christian Bassogog.
Sasa Cameroon itavaana katika fainali na mafarao wa Misri ambao walikuwa tayari wamejikatia tiketi ya fainali hiyo baada ya kuigaragaza Burkina Faso hapo juzi kwa mikwaju ya penalti.
Mchezo huo wa fainali ambao utafunga pazia la mashindano hayo ya soka ya kombe la mataifa ya Afrika utafanyika siku ya Jumapili.
Misri imeweka rekodi kwa kufanikiwa kufuzu kwa mara ya tisa kuingia fainali za kombe la Afrika.
Aidha imetwaa kombe hilo mara saba na hivyo kuwa nchi pekee barani Aafrika iliyolibeba kombe hilo mara nyingi zaidi.