Wanajeshi wa Nigeria waliotumwa Gambia kurejea nyumbani karibuni
Askari wa jeshi la Nigeria waliokuwa wametumwa nchini Gambia ili kuhakikisha usalama katika mchakato wa kushika madaraka serikali mpya ya nchi hiyo wanatazamiwa kurejea nchini mwao hivi karibuni.
Nigeria ilipeleka askari 200 pamoja na ndege kadhaa za kivita huko nchini Gambia katika operesheni ya nchi za magharibi mwa Afrika iliyokuwa na lengo la kudhamini usalama wakati wa kushika hatamu za madaraka serikali mpya ya Banjul baada ya kufanyika uchaguzi wa rais.
Spika wa bunge la wawakilishi la Nigeria, Yakubu Dogara ameashiria ushiriki wa jeshi la nchi hiyo katika kufanikisha mchakato wa kushika hatamu za uongozi rais mpya wa Gambia Adama Barrow na kueleza kwamba wanajeshi wa Nigeria wataondoka nchini humo karibuni.
Baada ya kuchachamaa kwa muda na kukataa kukabidhi hatamu za uongozi wa nchi, aliyekuwa rais wa Gambia Yahya Jammeh hatimaye alikubali matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika Desemba mosi mwaka jana na kungátuka madarakani kufuatia mashinikizo ya kieneo na kimataifa. Jammeh, ambaye aliitawala Gambia kwa muda wa miaka 22 ameondoka nchini humo na sasa yuko uhamishoni nchini Guinea ya Ikweta…/