Marekani yaahidi kuipatia silaha Nigeria
Serikali ya Nigeria imo mbioni kutafuta msaada wa silaha kwa Marekani.
Ofisi ya Rais wa Nigeria imetoa taarifa na kutangaza kuwa Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais Donald Trump wa Marekani kuhusiana na kustawishwa ushirikiano wa kijeshi kati ya Washington na Abuja.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa katika mazungumzo hayo, Trump amemhakikishia Buhari kuwa Marekani iko tayari kuipatia silaha Nigeria kwa ajili ya kupambana na ugaidi.
Itakumbukwa kuwa katika kipindi cha utawala wa aliyekuwa rais wa Nigeria Goodluck Jonathan, Marekani ilisimamisha uuzaji silaha na utoaji mafunzo kwa askari wa jeshi la Nigeria kutokana na wasiwasi wa tuhuma za ukiukaji wa haki za binadamu zilizokuwa zikiikabili serikali ya nchi hiyo.
Tangazo la Marekani la kuwa tayari kuipatia msaada wa silaha Nigeria linatolewa katika hali ambayo mnamo mwezi Desemba mwaka 2015 jeshi la nchi hiyo lilishambulia msikiti na kituo cha kidini cha Baqiyatullah katika mji Zaria na kumtia mbaroni kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria Sheikh Ibrahim Zakzaky, mkewe na makumi ya wanachama wa harakati hiyo baada ya kuwaua shahidi mamia ya Waislamu waliokuwa kwenye shughuli ya kidini.../