Mamia ya Wasomalia wapoteza maisha kwa maradhi ya kipindupindu
Waziri Mkuu wa Somalia ametangaza kuwa zaidi ya watu 100 wamefariki dunia nchini humo kutokana na ugonjwa wa kipindupindu.
Hassan Ali Khayre amesema kuwa, ugonjwa wa kipindupindu uliolikumba eneo la Bay, kusini magharibi mwa Somalia umesababisha kwa akali vifo vya watu 110 katika kipindi cha siku mbilizi zilizopita. Kwa mujibu wa Hassan Ali Khayre, watu wengine wengi wapo katika hali mbaya.
Ameongeza kuwa, maafa hayo ya kibinadamu yamesababishwa na ukosefu wa maji na ukame mkali ulioikumba nchi hiyo ya Pembe ya Afrika na kwamba serikali inalipa uzito suala la utatuzi wa mgogoro huo.
Wakati huo huo Mohammed Hassan Faqihi, mmoja wa viongozi wa jimbo la kusini magharibi mwa Somalia ametangaza kuwa, hali ya watu waliopatwa na ugonjwa huo wa kipindupindu katika eneo hilo haiwezi kudhibitiwa na ametaka msaada wa dharura kwa serikali na jamii ya kimataifa.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa zimechukuliwa hatua kadhaa za kukabiliana na baadhi ya changamoto zilizopo, ikiwa ni pamoja na kutuma timu ya misaada, dawa na vifaa vya tiba nchini Somalia.
Tangu mwezi Januari mwaka huu zaidi ya kesi 6000 za ugonjwa wa kipindupindu na kadhalika kesi 2500 za ugonjwa wa surua zimeripotiwa nchini Somalia.