Wamisri waandamana nchi nzima dhidi ya serikali kulalamikia kuwekwa mgao wa mikate
(last modified Thu, 09 Mar 2017 07:52:05 GMT )
Mar 09, 2017 07:52 UTC
  • Wamisri waandamana nchi nzima dhidi ya serikali kulalamikia kuwekwa mgao wa mikate

Raia wa Misri wamefanya maandamano dhidi ya serikali katika mikoa tofauti ya nchi hiyo, kulalamikia hatua ya kuwekwa mgao katika upatikanaji wa mikate nchini humo.

Habari kutoka Misri zinasema kuwa, maandamano hayo dhidi ya serikali yameitishwa kulalamikia hatua ya kuwekwa mgao wa mikate na kupunguzwa kiwango kilichotengwa kwa ajili ya mkate kwa kila raia wa nchi hiyo, ambapo wametoa nara dhidi ya serikali ya Rais Abdel Fattah el-Sisi. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia kubwa ya waandamanaji walikuwa wamebeba mabango yaliyokuwa na jumbe zinazosema: "Mimi siye Ikhwan, mimi nina njaa."

Utengenezaji wa mkate huko Misri

Hii ni katika hali ambayo serikali ya Cairo iliitangaza harakati ya Ikhwanul Muslimin kuwa ya kigaidi sambamba na kuwatia jela viongozi wake wengi hadi sasa. Kadhalika Wamisri wametaka kurejeshwa madarakani Bassem Ouda, Waziri wa Ustawi wa kipindi cha Muhammad Mursi, rais wa zamani wa Misri aliyeondolewa madarakani kwa nguvu na makamanda wa jeshi na kutiwa jela. Wamisri wanaamini kuwa katika kipindi cha Ouda, kulishuhudiwa ustawi na uthabiti wa bei za bidhaa madukani. Aidha waandamanaji wenye hasira katika mikoa ya Alexandria, Damanhur na Kafr El Sheikh walifunga njia za reli na hivyo kupelekea treni kusitisha shughuli zake.

Wamisri wenye hasira kali

Mjini Cairo waandamanaji walifunga barabara ya al-Nil na hivyo kusababisha msongamano wa magari. Kufuatia hali hiyo, Ali El-Sayed Ali Al-Moselhi Waziri wa Ustawi wa sasa ameitisha kikao na waandishi wa habari na kusema kuwa, serikali inafanya juhudi ili kukidhi matakwa ya wananchi na kuwadhaminia mahitaji yao.

Bassem Ouda, Waziri wa Ustawi wa kipindi cha Muhammad Mursi, ambaye wananchi wanamtaka

Weledi wa mambo wameandika katika mitandao ya kijamii kwamba matukio ya sasa ya nchi hiyo yanaashiria kumalizika subira ya Wamisri kutokana na kupanda gharama za maisha nchini humo. Aidha wameonya juu ya kutokea mapinduzi kama yale ya mwaka 2011 yaliyopelekea kuondolewa madarakani dikteta wa zamani wa nchi hiyo, Hosni Mubarak.