Kimbunga, maporomoko ya ardhi vyaua watu 16 kisiwani Madagascar
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i26194-kimbunga_maporomoko_ya_ardhi_vyaua_watu_16_kisiwani_madagascar
Kwa akali watu 16 wameaga dunia kufuatia maporomoko ya ardhi katika eneo la Vatomandry, mashariki mwa Madagascar.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 10, 2017 10:36 UTC
  • Kimbunga, maporomoko ya ardhi vyaua watu 16 kisiwani Madagascar

Kwa akali watu 16 wameaga dunia kufuatia maporomoko ya ardhi katika eneo la Vatomandry, mashariki mwa Madagascar.

Maporomoko hayo ya ardhi yanaripotiwa kusababishwa na mvua kubwa iliyonyesha jana Alkhamisi na kimbunga kilichokikumba kisiwa hicho Jumanne iliyopita.

Duru za habari zinasema Kimbunga cha Enawo kimesababisha vifo vya watu tisa huku makumi ya maelfu ya wengine wakiachwa bila makao katika kisiwa cha Madagascar.

Kimbunga Enawo kisiwani Madagascar

Ofisi ya Taifa ya Kupambana na Majanga huko Madagascar (BNGC) imesema kuwa, watu zaidi ya elfu 20 wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na athari za kimbunga hicho.

Shirika la Msalaba Mwekundu limeonya kuwa, huenda athari zaidi za janga hilo la kimaumbile zikashuhudiwa katika siku zijazo.

Itakumbukwa kuwa, mwaka 2012, kimbunga cha Irina na tufani ya Giovanna vilisababisha vifo vya watu zaidi ya 100 nchini Madagascar.