Idadi ya waliouawa na kimbunga Madagascar yapindukia 50
Idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na Kimbunga cha Enawo katika kisiwa cha Madagascar imepindukia watu 50.
Idara ya Kukabiliana na Majanga nchini humo BNGRC imesema mbali na maafa hayo ya makumi ya watu, janga hilo la kimaumbile limesababisha watu karibu laki 2 waachwe bila makazi.
Mkuu wa idara hiyo Thierry Venty amesema kuwa, serikali imezindua nyumba 137 za muda kwa ajili ya kuwahifadhi waathiriwa wa kimbunga hicho.
Shirika la Msalaba Mwekundu limeonya kuwa, kimbunga hiki ni kikubwa kuwahi kushuhudiwa katika kisiwa hicho kilichoko kusini mashariki mwa bara Afrika tangu mwaka 2012 na huenda kitaathiri watu zaidi ya laki 7.
Idara ya Hali ya Hewa ya Madagascar imetangaza kuwa, kimbunga cha "Enawo" kimepungua makali yake kwa kuwa na mawimbi ya kasi ya kilomita 45 hadi 50 kwa saa.
Itakumbukwa kuwa, mwaka 2012, kimbunga cha Irina na tufani ya Giovanna vilisababisha vifo vya watu zaidi ya 100 nchini Madagascar.