Mahakama Nigeria yaanza kusikiliza kesi ya kiongozi wa Boko Haram
Mahakama ya Abuja nchini Nigeria jana ilisikilizi kesi inayomkabili kiongoni mmoja wa ngazi za juu wa kundi la kigaidi la Boko Haram na wenzake kadhaa wanaokabiliwa na tuhuma za kuteka nyara na kuua raia kumi wa nchi za kigeni.
Kesi hiyo imefunguliwa dhidi ya Khalid al-Barnawi na wenzake 6 wa kundi la Ansaru ambalo ni tawi la kundi la kigaidi la Boko Haram.
Khalid al-Barnawi pia amewekwa kwenye orodha ya magaidi hatari duniani wanaosakwa na Marekani.
Al Barnawi na wenzake wanatuhumiwa kuwa walihusika na mauaji ya raia wa kigeni katika kipindi cha kati ya mwaka 2011 na 2013 wakiwemo raia wawili wa Italia na Uingereza, Franco Lamolinara na Chris McManus.
Kundi la kigaidi la Boko Haram limekuwa likifanya mauaji ya kutisha katika maeneo ya kaskazini na kaskazini mashariki mwa Nigeria kwa miaka saba sasa. Takwimu zinasema zaidi ya watu elfu 20 wameuawa na mamilioni ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi tangu kundi hilo livamie maeneo ya kaskazini mwa Nigeria mwaka 2009.