Wapinzani waandamana Zimbabwe, wadai kuna njama za kuiba kura
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i26710-wapinzani_waandamana_zimbabwe_wadai_kuna_njama_za_kuiba_kura
Maelfu ya wafuasi wa vyama vya upinzani nchini Zimbabwe wameshiriki maandamano katika mji mkuu Harare, kulalamikia kile wanachodai kuwa ni njama ya kuiba kura katika uchaguzi ujao wa rais.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 22, 2017 11:12 UTC
  • Wapinzani waandamana Zimbabwe, wadai kuna njama za kuiba kura

Maelfu ya wafuasi wa vyama vya upinzani nchini Zimbabwe wameshiriki maandamano katika mji mkuu Harare, kulalamikia kile wanachodai kuwa ni njama ya kuiba kura katika uchaguzi ujao wa rais.

Wakiongozwa na Mchungaji Evan Mawarire, kiongozi wa harakati ya malalamiko ya wananchi nchini Zimbabwe ambaye hivi karibuni alitangaza kuwa atagombea kiti cha rais dhidi ya Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo katika uchaguzi unaotazamiwa kufanyika mwakani, waandamanaji hao wameitahadharisha Tume ya Uchaguzi nchini dhidi ya kufanya njama yoyote ya kuchakachua matokeo ya uchaguzi huo.

Viongozi wengine wa upinzani walioongoza maandamano hayo ni pamoja na Morgan Tsvangirai, kinara wa chama cha MDC, Jacob Mafume, msemaji wa chama cha People's Democratic Party, Maureen Kademamaunga wa vuguvugu la "She Votes" na Promise Mkhwananzi  wa harakati ya Tajamuka.

Maandamano ya wapinzani Zimbabwe

Waandamanaji hao walikusanyika katika Medani ya Uhuru kabla ya kuandamana hadi katika jengo la Tume ya Uchaguzi ambapo walisikika wakitoa nara za kumtaka mwenyekiti wa tume hiyo Rita Makarau ajiuzulu.

Kiongozi mkongwe wa upinzani nchini humo, Morgan Tsvangirai ameifananisha Tume ya Uchaguzi ZEC na refarii ambaye ameamua kuweka filimbi chini na kisha kuanza kuichezea timu moja kati ya mbili zinazochuana, akisisitiza kuwa, kuna haja ya kufanyiwa marekebisho mfumo wa uchaguzi nchini humo kabla ya uchaguzi mkuu wa mwakani.

Licha ya takriban viongozi wa vyama vyote vya upinzani nchini Zimbabwe kushiriki maandamano ya leo, lakini Joyce Mujuru, mkuu wa chama cha PDP hakushiriki maandamano hayo wala kuwakilishwa na afisa yeyote wa chama.

Rais Mugabe wa Zimbabwe

Rais Mugabe mwenye umri wa miaka 93 na ambaye amekuwa madarakani nchini Zimbabwe tangu mwaka 1980, amekuwa akisisitiza kuwa yupo tayari kutetea kiti chake katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2018.