Tahadhari kuhusu hali ya mgogoro katika nchi za mashariki mwa Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i26926-tahadhari_kuhusu_hali_ya_mgogoro_katika_nchi_za_mashariki_mwa_afrika
Mgogoro wa ukame katika eneo la mashariki mwa Afrika umeulazimisha Umoja wa Mataifa kutoa onyo kuhusiana na hatari ya janga la wakimbizi kwenye eneo hilo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 27, 2017 12:01 UTC
  • Victoria Akyeampong, mkuu wa kamisheni ya wakimbizi ya Umoja wa Mataifa UNHCR katika eneo la mashariki mwa Afrika
    Victoria Akyeampong, mkuu wa kamisheni ya wakimbizi ya Umoja wa Mataifa UNHCR katika eneo la mashariki mwa Afrika

Mgogoro wa ukame katika eneo la mashariki mwa Afrika umeulazimisha Umoja wa Mataifa kutoa onyo kuhusiana na hatari ya janga la wakimbizi kwenye eneo hilo.

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya wakimbizi ametoa tamko na kusema kwamba, hali ya wakimbizi katika nchi za mashariki mwa Afrika inasikitisha mno na kuna udharura wa kuchukuliwa hatua madhubuti za kuzuia kutokea maafa ya kibinadamu kwenye eneo hilo.

Victoria Akyeampong, mkuu wa kamisheni hiyo katika eneo la mashariki mwa Afrika amebainisha kuwa, hali ya kusikitisha mno ya wakazi wa maeneo hayo inasababishwa na migogoro ya ndani pamoja na ukame uliolikumbwa eneo la Afrika Mashariki na kufikia hadi katika nchi zinazopakana na maziwa makuu.

Amesema, kuna wajibu wa kutafutwa njia mwafaka za kukabiliana na janga hilo na kutekelezwa mbinu madhubuti na kamili za kupambana na mgogoro huo ukiwemo wa wakimbizi. 

Askari wenye silaha wakipita karibu na mifugo iliyoteketea kwa ukame nchini Somalia

 

Ijapokuwa ukame, njaa na kulazimika watu kuhama maeneo yao kutokana na mapigano ya ndani yanatajwa kuwa ni changamoto kuu za kila siku za nchi za Afrika Mashariki, lakini hivi sasa changamoto hizo zimefikia hali mbaya na ya kutisha.

Kiwango kidogo sana cha mvua, kupoteza rutuba ardhi za kilimo, mabadiliko ya hali ya hewa, misingi  na mikakati dhaifu ya kiuchumi, kutodhibitiwa ongezeko la watu na vita vya kikabila na vya baina ya serikali na makundi yenye silaha sambamba na kuweko magenge ya kigaidi ni miongoni mwa sababu za kuongezeka njaa, ukame na watu kuyakimbia makazi yao barani Afrika.

Maeneo mengi ya Somalia hivi sasa yamekumbwa na ukame mkubwa na sababu hasa ya jambo hilo  ni kuweko genge la kigaidi la al Shabab katika maeneo hayo. Idadi kubwa ya watu wa sehemu hizo wamelazimika kuacha maeneo yao ya kilimo na makazi yao na kukimbilia maeneo mengine ya ndani na nje ya Somalia. Kama tunavyojua,  uvamizi wa watu wengi kwenye maeneo hayo kunakokwenda sambamba na kutumiwa vibaya mazingira ya maeneo hayo, kumesababisha kukatwa miti ovyo, ukame, uchache wa mvua na kupungua chakula.

Hali ni hiyo hiyo pia katika maeneo ya nchi nyingine. Kwa mfano mgogoro wa kisiasa nchini Burundi uliozuka baada ya Rais Piere Nkurunziza kung'ang'ania madaraka, umepelekea Burundi kutengwa na katika upande mwingine, raia wa nchi hiyo wamelazimika kukimbilia maeneo mengine hasa ya nje ya nchi. Huko Ethiopia, Madagascar na baadhi ya nchi za eneo hilo pia mabadiliko ya hali ya hewa yamesababisha ukame mkubwa. 

Rais Pierre Nkunziza wa Burundi

 

Hali hiyo imejitokeza katika mazingira ambayo taasisi na mashirika ya kimataifa yanatosheka tu na kutoa ripoti za tahadhari, misaada michache na kusisitizia udharura wa kutolewa misaada ya kibinadamu, lakini yanashindwa kusimamia mapambano dhidi ya hali hiyo. Ukosefu wa usalama katika baadhi ya maeneo hayo unawafanya watoaji misaada washindwe kuwafikia watu wenye shida na katika upande mwingine, nchi nyingi za Magharibi hazitekelezi ahadi zao za misaada ya fedha kwa mashirika hayo ya kimataifa na hivyo kukwamisha kazi za mashirika hayo.

Ijapokuwa misaada ya nyakati tofauti inasaidia kwa kiasi fulani kupunguza janga na maafa ya kibinadamu kwenye maeneo hayo, lakini inaonekana wazi kuwa kunahitajia juhudi za kweli na kubwa zaidi za kufanikisha kazi hiyo. Kwanza ni suala la usalama. Katika hili la usalama, kuna wajibu wa kuchukuliwa hatua za kweli za kukomesha mizozo na mapigano ya ndani na yale ya magenge ya kigaidi. Bila ya shaka yoyote ushirikiano wa kweli baina ya nchi za eneo hilo unaweza kwa kiwango fulani kurejesha utulivu kwenye maeneo hayo. 

Mapendekezo mengine yanayotolewa na weledi wa mambo ni wajibu wa kuangaliwa upya siasa za kiuchumi na uwekezaji wa muda mrefu katika sekta ya kilimo na vile vile kutumiwa zana za kisasa na mbinu bora za kilimo, mbegu zenye uzalishaji mkubwa na mbinu za kileo za umwagiliaji maji kama njia ya kuwadhaminia usalama wa chakula wakazi wa maeneo hayo.