Maafisa polisi zaidi ya 140 wa Rwanda wawasili nchini Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i27320-maafisa_polisi_zaidi_ya_140_wa_rwanda_wawasili_nchini_sudan_kusini
Rwanda imetuma makumi ya maafisa wa polisi wa kikosi kipya cha maafisa wake wa kulinda amani nchini Sudan Kusini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 05, 2017 03:13 UTC
  • Maafisa polisi zaidi ya 140 wa Rwanda wawasili nchini Sudan Kusini

Rwanda imetuma makumi ya maafisa wa polisi wa kikosi kipya cha maafisa wake wa kulinda amani nchini Sudan Kusini.

Bosco Rangira, Naibu Kamishna wa Polisi ya Rwanda amesema maafisa 144 wa polisi ya nchi hiyo walioondoka mjini Kigali jana Jumanne, watahudumu chini ya mwavuli wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa UNMISS.

Afisa huyo wa mkuu wa polisi wa Rwanda ameongeza kuwa, maafisa hao kutoka Kikosi cha Polisi cha Formed Police Unit (FPU) wataungana na askari wenzao 240 na washauri wa polisi 29 wa Rwanda ambao kwa sasa wanafanya kazi chini ya UNMISS.

Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa Sudan Kusini UNMISS

Kabla ya kuondoka, Emmanuel K. Gasana, Inspekta Jenerali wa Polisi wa Rwanda aliwataka maafisa hao kufanya kazi kwa kujituma na kwa kuonyesha nidhamu ya hali ya juu. Rwanda ina takriban askari polisi wa kulinda amani 1,200 katika nchi za Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Haiti.

Kutokana na kushadidi machafuko, ukame na baa la njaa, mamia ya maelfu ya raia wa Sudan Kusini wameikimbia nchi na sasa wanaishi kama wakimbizi katika nchi jirani kama Sudan na Uganda.

Hapo jana raia zaidi ya elfu 3 wa Sudan Kusini waliingia katika nchi jirani ya Uganda baada ya wanajeshi wa serikali SPLA kuvamia mji wa mpakani wa Pajok, na kuanza kufanya mauaji kiholela.