Magaidi watano wa Al-Shabab waliohukumiwa kifo Puntland, Somalia wanyongwa
Eneo la Somalia la Puntland lenye mamlaka yake ya ndani limetekeleza adhabu ya kifo kwa watu watano wanaoaminika kuwa wanamgambo wenye misimamo ya kufurutu mpaka waliohusika na mauaji ya maafisa watatu waandamizi wa serikali ya eneo hilo.
Mwenyekiti wa mahakama ya kijeshi ya Puntland Abdifatah Haji Aden alisema jana watu hao, ambao ni wanamgambo wa kundi la kigaidi la Al-Shabab, walihusika na mauaji ya Mkurugenzi wa Ikulu ya Rais, Mkuu wa Mashtaka wa mahakama ya kijeshi na Naibu Kamanda wa Polisi. Mauaji hayo yalifanywa mwezi Desemba mwaka jana katika mji wa bandari wa Bossaso.
"Walimuua naibu kamanda wa polisi wa Bossaso, mkurugenzi wa ikulu ya Puntland na mwendesha mashtaka wa Bossaso", amefafanua mwenyekiti huyo wa mahakama ya kijeshi.
Kwa mujibu wa Aden, watu hao walikiri kuwa ni wanamgambo wa kundi la kigaidi la Al-Shabab na kwamba walihusika na mauaji ya maafisa hao wa serikali ya Puntland. Ameongeza kuwa hukumu yao ilikwisha pitishwa tokea kabla na kwamba jana ilikuwa siku ya utekelezaji wake tu.
Kundi la kigaidi la Al-Shabab linaendesha uasi unaolenga kuvitimua vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika vilivyoko nchini Somalia AMISOM, kuiangusha serikali ya nchi hiyo na kuunda kile linachodai kuwa ni 'utawala wa Kiislamu' katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Kwa mujibu wa wataalamu na maafisa wa serikali, harakati za kundi la kigaidi la Al-Shabab sasa zimepamba moto katika eneo la Puntland baada ya kutimuliwa kwenye ngome zao kusini mwa Somalia na vikosi vya AMISOM vikishirikiana na jeshi la nchi hiyo…/