Apr 16, 2017 07:14 UTC
  • Wimbi la mauaji laendelea Sudan Kusini, 14 wauawa

Kwa akali watu 14 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika mapigano mapya baina ya wanajeshi wa serikali na waasi katika mji wa Raga nchini Sudan Kusini.

Msemaji wa kundi kuu la waasi katika eneo hilo, Lam Paul Gabriel Lam amedai kuwa, katika kipindi cha siku mbili zilizopita, serikali imewalenga wakaazi wa mji huo kwa mabomu na silaha nyingine.

Amesema watu zaidi ya 14 wameuawa katika hujuma hizo za serikali huku wengine wengi wakijeruhiwa, mbali na nyumba zao kuteketezwa moto.

Santo Domic Chol, Msemaji wa Jeshi la Sudan Kusini amekwepa kulizungumzia suala hilo alipotakiwa kufanya hivyo na shirika la habari la Reuters.

Waasi Sudan Kusini

Mauaji haya yanaripotiwa wiki moja baada ya watu wengine 16 kuuawa katika mapigano baina ya wanajeshi wa serikali na waasi katika mji wa Wau nchini Sudan Kusini. 

Hayo yalikuwa makabiliano makali ya pili kushuhudiwa katika siku za hivi karibuni nchini humo, haswa kwa kuzingatia kuwa mapigano mengine kati ya askari wa serikali ya Juba na magenge ya waasi yalishuhidiwa hivi karibuni katika mji wa Pajok.

Kutokana na kushtadi mfululizo wa mauaji na mapigano mapya nchini Sudan Kusini, Noriko Yoshida, mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) ametahadharisha kuhusu kuongezeka wimbi la wakimbizi wanaoikimbia nchi hiyo changa zaidi barani Afrika. Amesema kuwa, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2017, inakadiriwa kuwa wakimbizi laki moja na elfu 80 raia wa Sudan Kusini wataingia nchini Sudan.  

 

Tags