Kulaaniwa uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Zambia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i27892-kulaaniwa_uingiliaji_wa_marekani_katika_masuala_ya_ndani_ya_zambia
Sambamba na kuendelea vuta nikuvute ya kisiasa kuhusiana na uchaguzi uliopita nchini Zambia, Rais Edgar Lungu wa nchi hiyo ameashiria uingiliaji wa Marekani na Umoja wa Ulaya katika masuala ya ndani ya nchi hiyo hususan kutiwa mbaroni kiongozi wa wapinzani na kulaani vikali uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya Zambia.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 17, 2017 13:20 UTC
  • Kulaaniwa uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Zambia

Sambamba na kuendelea vuta nikuvute ya kisiasa kuhusiana na uchaguzi uliopita nchini Zambia, Rais Edgar Lungu wa nchi hiyo ameashiria uingiliaji wa Marekani na Umoja wa Ulaya katika masuala ya ndani ya nchi hiyo hususan kutiwa mbaroni kiongozi wa wapinzani na kulaani vikali uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya Zambia.

Rais Edgar Lungu amesisitiza kuwa, wanadiplomasia wa kigeni walioko nchini Zambia badala ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao yaliyowaleta nchini humo. Serikali ya Rais Edgar Lungu sanjari na kukataa kukutana na kiongozi wa upinzani Hakainde Hichilema imemtuhumu mwanasiasa huyo kwamba, ni mwenye hadaa na kwamba, imemtia mbaroni kwa kuhadaa fikra za waliowengi nchini humo.

Siku chache zilizopita Marekani na Umoja wa Ulaya zilitoa taarifa ambayo sambamba na kuonyesha wasiwasi wao kwa hatua hiyo ya serikali ya Zambia zilitoa wito wa kupunguzwa vuta nikuvute ya kisiasa katika nchi hiyo ya Kiafrika. Jack Mwiimbu wakili wa Hakainde Hichilema kiongozi wa upinzani wa Zambia amesema kuwa, kutiwa mbaroni kiongozi huyo wa upinzani kuliambatana na utumiaji mabavu na kwamba, polisi walivunja mlango wa mteja wake na kisha kurusha mabomu ya kutoa machozi. Uchaguzi wa Zambia ulifanyika Agosti 11 mwaka jana na kuambatana na mivutano mikubwa. Katika uchaguzi huo wagombea 9 walijitokeza kuwania kiti cha Urais ambapo mchuano mkali ulishuhudiwa kati ya Rais Edgar Lungu na Hakainde Hichilema kiongozi wa chama cha upinzani cha United Party for National Development.

Hakainde Hichilema kiongozi wa chama cha upinzani cha United Party for National Development

Katika hali ambayo, matokeo ya awali ya uchaguzi huo yalionyesha kuwa, Hakainde Hichilema anaongoza, lakini matokeo yaliyokuja kutangazwa na Tume ya Uchaguzi yalionyesha kuwa, Rais Edgar Lungu ndiye aliyekuwa mshindi wa kiti cha Urais baada ya kujikusanyia asilimia 50 ya kura. Kutangazwa matokeo hayo kuliifanya Zambia igubikwe na wimbi la mvutano ambapo  makumi ya mamia ya wafuasi wa Hakainde Hichilema walimiminika katika mitaa na barabara za nchi hiyo ambapo walivamia majengo ya serikali na kulalamikia kile walichokiita kuwa "wizi wa kura na uchakachuaji wa matokeo ya uchaguzi huo." Idadi kadhaa ya wapinzani walitiwa mbaroni na vikosi vya usalama vya Zambia.

Malalamiko hayo yalishadidi zaidi wakati Hakainde Hichilema alipotangaza kwamba, hayakubali matokeo ya uchaguzi huo kwa namna yoyote ile huku chama chake cha United Party for National Development kikiwasilisha ombi la kutaka kuhesabiwa tena kura za uchaguzi huo. Akihutubu baada ya kutangazwa mshindi, Rais Lungu aliwataka wananchi wa Zambia na wapinzani wa nchi hiyo wawe na subira na walinde utulivu.

Uchaguzi wa Zambia  Agosti 2016

Pamoja na hayo mvutano na upinzani ni mambo ambayo yameendelea kushuhudiwa licha ya kupita miezi kadhaa tangu kuanza kazi serikali ya Rais Lungu. Hakainde Hichilema  mchumi na mfanyabiashara tajiri wa nchi hiyo alijitosa katika kinyang'anyiro cha uchaguzi akipiga nara za kuhitimishwa ufisadi na utawala wa kipolisi nchini Zambia. Hata katika kipindi cha baada ya uchaguzi huo, mfanyabiashara huyo ameendeleza upinzani wake dhidi ya serikali. Katika hali ambayo, Zambia inahesabiwa kuwa moja ya nchi zenye uthabiti wa kidemokrasia barani Afrika na ambayo inategemea zaidi pato lake kupitia utalii na kuvutia wawekezaji wa kigeni, bila shaka kuendelea vurugu na ukosefu wa uthabiti wa aina yoyote ni kengele ya hatari kwa mustakabali wa nchi hiyo.

Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana Rais wa Zambia akasisitiza juu ya kudumishwa umoja na mshikamano baina ya matabaka mbalimbali ya wananchi. Hata hivyo kutiwa mbaroni Hakainde Hichilema kiongozi wa upinzani wa Zambia kumeifanya nchi hiyo ikabiliwe na mgogoro mpya. Baadhi ya wapinzani wa serikali ya Zambia na asasi za kutetea haki za binadamu nchini humo wamelaani kutiwa mbaroni Hakainde Hichilema na kuitaja hatua hiyo kwamba, ni ukiukaji wa sheria na ukanmfamizaji wa anga huru ya kisiasa. Hii ni katika hali ambayo, Rais Lungu amepinga madai yote hayo na kubainisha kwamba, chimbuko la upinzani dhidi ya serikali yake ni uingiliaji wa kigeni hususan wa madola ya Magharibi na Marekani ambayo yanataka kuwa na satua na upenyezaji zaidi katika nchi hiyo na kulitumia suala hilo kwa ajili ya kudhamini maslahi yao.